Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (wa kwanza kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari (wa pili kulia) walipomkaribisha Waziri wa Nchi anaeshughulikia TEHAMA na Ulinzi-Uganda Mhe. Kabbyanga Godfrey (katikati) kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma-TCRA Bi. Lucy Mbogoro. Picha na TCRA)
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt Jabiri Bakari (kushoto) akiwa sambamba na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili katikati) wakimkaribisha Waziri wa Nchi anaeshughulikia TEHAMA na Ulinzi-Uganda Mhe. Kabbyanga Godfrey aliefika TCRA kwa ziara ya mafunzo akiambatana na Maafisa Waandamizi wa Tume ya Mawasiliano Uganda(UCC) (hawamo pichani). Wa kwanza kulia anaeshuhudia ni Msaidizi wa Waziri wa Uganda. PICHA NA TCRA Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akiperuzi jambo kwenye kijitabu wakati alipomkaribisha Mgeni wake Waziri wa Nchi anaeshughulikia TEHAMA na Ulinzi-Uganda Mhe. Kabbyanga Godfrey (anaesaini kitabu cha wageni kushoto) Waziri huyo wa Uganda alioongozana ujumbe wa maafisa wa Tume ya Mawasiliano Uganda (UCC) waliokuja Tanzania kwa ziara ya mafunzo ya usimamizi wa sekta ya Mawasiliano kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ikiwa ni mkakati wa kuboresha Sheria ya Mawasiliano ya nchini kwao. Picha na TCRA)
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kundo Mathew (kushoto), akimweleza jambo Waziri wa Nchi anaeshughulikia TEHAMA na Ulinzi-Uganda Mhe. Kabbyanga Godfrey aliefika Tanzania kwa ziara ya mafunzo. Katika tukio hili anakaribishwa kujifunza kutoka TCRA namna Sheria za Mawasiliano zinavyowezesha usimamizi wa Sekta ya mawasiliano nchini. PICHA NA TCRA
**************************
Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeihakikishia Uganda kuwa itaendelea kuipa ushirikiano katika kujenga uwezo wa usimamizi wa sekta ya Mawasiliano na TEHAMA, sambamba na kudumisha ushirikiano wa kitaalam katika usimamizi wa sekta hizo.
Akizungumza wakati alipoukaribisha ujumbe wa Tume ya Mawasiliano Uganda (UCC) ukiongozwa na Waziri wa Nchi anaeshughulikia Ulinzi na TEHAMA Mheshimiwa Kabbyanga Godfrey uliofika katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa ziara ya Mafunzo na kubadilishana ujuzi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Andrew Mathew alibainisha kuwa, Tanzania imefanikiwa kusimamia vilivyo sekta ya Mawasiliano kwa kuweka Sera Madhubuti za usimamizi wa huduma za Mawasiliano, huku akiwahakikishia wageni fursa tele ya kujifunza katika sekta ya Mawasiliano.
“Tanzania imepitisha sera zinazounga mkono ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano - TEHAMA na mfumo wa kisheria na udhibiti unaounga mkono ukuzaji wa uchumi wa kidijiti,” alisisitiza Kundo na kuongeza kuwa “Ninakuhakikishia ujumbe wako kwamba utapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu ambao utakuwa muhimu katika marekebisho ya Sheria yenu ya Mawasiliano ya 2013,” alibainisha.
Kwa upande wake Waziri Kabbyanga akishukuru baada ya ukaribisho alimweleza Naibu Waziri Kundo, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari na Menejimenti ya TCRA lengo la ziara yao Tanzania kuwa ni kujifunza zaidi namna Tanzania inavyosimamia huduma za Mawasiliano ambao ziara yao mahususi katika ofisi za TCRA ililenga kujifunza namna Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inavyowezesha usimamizi wa sekta ya Mawasiliano.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili kwenye ofisi za TCRA jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi anaeshughulikia Ulinzi na TEHAMA Mheshimiwa Kabbyanga Godfrey alimweleza mgeni wake Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Mheshimiwa Kundo Mathew kwamba Uganda imeona vema kuja kujifunza Tanzania kwa kuzingatia ujirani na namna ambavyo Tanzania imefanikiwa katika kusimamia na kudhibiti sekta ya Mawasiliano.
“Tumeambiwa kwamba Tanzania mnazo Sheria Madhubuti za usimamizi wa sekta ya mawasiliano Tumekuja hapa kwa sababu mazingira yetu ni sawa na ya Tanzania hivyo tumeona hapa kwenu tutajifunza na kupata maarifa yenye uhalisia zaidi, tofauti na tungeamua kwenda kujifunza sehemu nyingine,” alisisitiza Kabbyanga.
Alieleza kwamba pia Uganda inanuia kuboresha huduma za Mawasiliano ya simu kwa raia wake hivyo imeamua kuja Tanzania kujifunza katika eneo linalohusu Mawasiliano ya simu.
Ziara ya Tume ya Mawasiliano Uganda kuzuru Tanzania, na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni mwendelezo wa Mamlaka mbalimbali za Usimamizi wa Mawasiliano za Afrika kufika Tanzania kujifunza na kubadilishana ujuzi wa usimamizi wa huduma za Mawasiliano. Miongoni mwa nchi nyingine zilizozuru TCRA mwaka huu ni pamoja na Malawi, Zimbabwe, Burundi, Rwanda, Uganda, na Msumbiji.