Tuesday, 30 April 2019

Polisi Njombe yaua majambazi wawili, mmoja atoroka

Na Amiri kilagalila-Njombe
Jeshi la Polisi Mkoani Njombe limefanikiwa kuwaua majambazi wawili kati ya watatu waliokuwa wakijaribu kupora mali kwa kutumia Jambia,kisu na Panga.

Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoa wa Njombe ACP Salum Hamduni,amesema tukio hilo limetokea kijiji cha Lupembe wilayani Njombe  April 28 majira ya saa 01:40 usiku ambapo watu wasiofahamika walivamia nyumba ya Esau Muhavile kwa kuvunja geti na mlango kwa kutumia Spring ya gari na kuingia ndani kwa nia ya kupora mali.

"Awali majira ya saa 01:30 usiku mlinzi aitwae Linus Matimbwi akiwa Lindoni alisikia vishindo vya watu kuzunguka nyumba hiyo na kumgongea Baraka mayemba mfanyakazi wa Esau na kumweleza kuwa huku nje hali si shwari ndipo Baraka akaamua kumpigia simu mkuu wa kituo kidogo cha polisi Lupembe kwa msaada"alisema kamanda.

Amesema kuwa Polisi waliwahi kufika katika eneo la tukio na kugundua kuwa majambazi hao wapo ndani na kupiga Risasi hewani kuwataarifu kuwa wapo chini ya ulinzi lakini hawakutii amri na matokeo yake jambazi mmoja wapo alirusha jambia na kumjeruhi mkuu wa kituo begani kitendo kilichopelekea Polisi kumpiga Risasi kifuani jambazi Newton Mbanga aliyerusha jambia huku Leonard Alphonce akipigwa risasi kichwani na kusababisha vifo vyao.

"Mbinu iliyotumika na majambazi hao ni kuvunja mlango kwa kutumia spring ya gari na kuingia ndani kwa nia ya kupora mali/pesa na watuhumiwa ambao ni majambazi wawili kati yao walifariki dunia na mmoja alifanikiwa kutoroka,na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo" aliongeza kusema kamanda.


Share:

Fisi Wazua Gumzo Na Kuwa Tishio Kahama

Kundi kubwa la  wanayama aina ya fisi limewajeruhi watu  watano  sehemu mbalimbali za miili yao katika  kata za  Nyandekwa na Kilago halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga wakati wakijaribu kupambana na fisi hao waliovamia makazi ya watu.
 
Diwani wa Kata ya Kilago PETER EMANUEL amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia  April 28,2019  ambapo  majeruhi watatu hali zao bado hazijaimarika na wanaendelea na matibabu katika hospitali ya mji wa Kahama  na kwamba wananchi katika maeneo hayo amejawa na hali ya wasiwasi.
 
Wakizungumza wakiwa wamelazwa katika hospitali ya mji wa Kahama, baadhi ya  majeruhi wameiomba serikali  kuwadhibiti fisi hao kwani wanaweza kuleta madhara makubwa kwa wananchi na kwamba wamekuwa wakipambana nao mara kwa mara.
 
Afisa maliasiri  halmashauri ya mji wa Kahama, THOMAS MANUMBU amesema  tatizo la Fisi kuvamia makazi ya watu   bado lipo kwa wingi katika kata za pembezoni tangu mwezi wa pili mwaka huu  huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati serikali inaendelea kupambana na    fisi hao.
 
Kwa upande wake Mhifadhi wa wanyanama Tanzania  (TAWA) wilaya ya Kahama, MAPANYA KARUTO  amewataka wananchi kutumia toshi nyakati za usiku na kwamba waondokane na imani za kishirikina  dhidi ya uwepo wa fisi hao.
 
 Credit;kahama Fm



Share:

Maandalizi Ya Sherehe Za Mei Mosi Yapamba Moto Sokoine Mbeya.

NA.MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amekagua maandalizi ya Sherehe za Mei Mosi na kusema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa.

Ametoa kauli hiyo Aprili 29, 2019 baada ya kupokea taarifa ya mbalimbali za Kamati ya Maandalizi walipokutana kujadili na kupanga mipango katika kuelekea kilele cha sherehe hizo zinazotarajiwa kuadhimishwa katika Viwanja vya Sokoine Jijini Mbeya.

Waziri amesema Kamati ya Mkoa kwa kushirikiana na Ofizi yake imeendelea na maandalizi hayo na kuendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kufika kwa wingi katika viwanja hivyo siku ya tarehe 1 Mei, 2019.

“Hadi sasa maandalzi yamefikia hatua nzuri na watu wanafanya kazi kwa umoja ili kuhakikisha shughuli hii inafana, wito wangu wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kuunga mkono wafanyakazi wa Tanzania katika siku yao hii muhimu.”Alisema waziri Mhagama.

Waziri aliwataka wanakamati hao wahakikishe wanasimamia vizuri wageni, pamoja na shughuli zote zitakazofanyika uwanjani hapo ili kuhakikisha wanaifikia siku hiyo kwa ushindi mkubwa.

Aidha Waziri aliongezea kuwa, uwepo wa maadhimisho hayo Jijini Mbeya wanachi wayatumie kama fursa ya kimaendeleo kwa kuwa mkoa utapokea wageni wengi hivyo waendelee kuwahudumia vyema.

Aidha kwa Upande wake rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya aliendelea kuhamasisha wananchi hususan wafanyakazi wote kujitokeza kwa wingi kuja kuiadhimisha siku hiyo.

 “Ni wakati sahihi kwa wafanyakazi wote nchini kuitumia siku hii maalum katika kuiadhimisha na kuienzi ikiwa ni sherehe ya upekee sana hivyo mjitokeze kwa wingi pamoja na wananchi wote kwa ujumla.”Alisisitiza Nyamhokya.

Maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi yatahadhimishwa Kitaifa katika Mkoa wa Mbeya ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli, aidha maonesho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo; Maandamano ya wafanyakazi na magari, Kwaya maalum, Nyimbo maalum kutoka kwa Vyama vya Wafanyakazi, wimbo maalum kutoka kwa wasanii wa kizazi kipya, vikundi vya ngoma kutoka mikoa mbalimbali, Nyimbo maalum kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kauli mbiu ya maonesha ya mwaka huu inasema; “Tanzania ya Uchumi wa Kati Inawezekana, Wakati wa Mishahara na Masilahi Bora kwa Wafanyakazi ni SASA”


Share:

Waziri Mhagama Awaasa Wafanyakazi Kutimiza Wajibu Wao

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista mhagama amewaasa wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii na uzalendo ili kuendelea kutimiza wajibu wao na kujiletea maendeleo nchini.

Ametoa kauli hiyo jana Aprili 29, 2019 alipokuwa akihutubia wafanyakazi walioshiriki katika semina maaalum ya wafanyakazi iliyowakutanisha wajumbe kutoka vyama mbali mbali vya wafanyakazi ili kujadili chimbuko la sherehe za wafanyakazi (Mei Mosi) na kujadili masuala ya sheria za kazi katika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.

Akizungumza na wajumbe wa semina hiyo, waziri Mhagama aliwaasa wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa weledi na tija ili kuendelea kuwa na taifa lenye maendeleo kwa kuzingatia mchango wa wafanyakazi nchini.

“Wafanyakazi endeleeni kufanya kazi kwa umoja, weledi huku mkizingatia kanuni, taratibu na sheria zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yenu pasipo kukiuka masuala ya msingi yanayowahusu,”alisema Waziri Mhagama.

Aliongezea kuwa, katika kuhakikisha Taifa linakuwa na maendeleo endelevu ni vyema wafanyakazi wakaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia mchango mkubwa wa wafanyakazi nchini katika kujiletea maendeleo kwa kuzingatia tija walioyonayo nchini.

“Niwakumbushe kuwa nyie ni wadau muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na Serikali inawategemea katika kuchangia maendeleo ya nchi hivyo mnapaswa kujali maeneo yenu ya kazi na kuendelea kuvitumia vyama vya wafanyakazi katika kueleza masuala yenu na kutumia vyama vyenu kutatua changamoto zinazowakabili,”alisisitiza Waziri Mhagama

Sambamba na hilo Waziri aliwataka wafanyazkai kuendelea kuzingatia uwajibikaji wenye misingi ya haki na usawa ili kuwa na mazingira salama ya kiutendaji pasipo kuvunja sheria za wafanyakazi ili kuwa na matokeo chanya kama inavyotarajiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUICO Taifa Bw. Paulo Sangeze alieleza shukrani zake kwa namna serikali inavyoendelea kuunga mkono uwepo wa Vyama vya wafanyakazi na kuahidi kutoa ushiorikiano kila itakapohitajika.

“Kwa dhati ya moyo wangu na kwa niaba ya TUCTA ninatoa shukrani kwa Serikali kwa namna inavyounga mkono shughuli za vyama vya wafanyakazi na hakika kumekuwa na mabadiliko makbwa tofauti na ilivyokuwa awali,”alisisitiza bw. Sangeze


Share:

Kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdad ajitokeza katika kanda ya video baada ya miaka 5

Kundi la kigaidi la Islamic State limesambaza mkanda wa video unaodai kumuonyesha kwa mara ya kwanza, baada ya kupita miaka mitano, kiongoza wa kundi hilo Ibrahim as-Samarrai, mashuhuri kama Abubakr al-Baghdadi.

Kundi hilo lilisambaza mkanda huo wa dakika 18 kupitia moja ya mitandao yake ya kijamii hapo jana Jumatatu ambapo kiongozi huyo wa magaidi ameonekana akizungumza na viongozi wengine watatu wa kundi hilo. 

Ukweli wa mkanda huo haukuweza kuthibitishwa mara moja na duru huru. Hata hivyo iwapo kutakuwa na ukweli wowote kwenye mkanda huo, kiongozi huyo wa magaidi atakuwa ameonekana hadhari kwa mara ya kwanza tokea mwaka 2014. 

Mwaka huo gaidi huyo alionekana kwenye mkanda mwingine akitoa hutuba katika moja ya misikiti ya mji wa Mosul, ulioko kaskazini mwa Iraq, akidai kwamba kundi hilo potovu lilikuwa limebuni mamlaka ya ukahlifa katika nchi hiyo na nchi nyingine jirani ya Syria.

As-Samarrai alionekana akizungumza katika mkanda huo wa kwanza baada ya kundi lake la kitakfiri kuteka na kudhibiti maeneo makubwa ya Iraq na Syria ambapo wahanga wengi waliuawa kinyama na kwa namna ya kutisha katika uvamizi huo. 

Licha ya kuwa tarehe ya kurekodiwa mkanda huo wa hivi karibuni haijaweza kuthibitishwa, lakini kiongozi huyo wa magaidi amesikika akizungumzia mashambulio ya kigaidi yaliyotekelezwa hivi karibuni huko Sri Lanka na kupelekea mamia ya watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa. 

Kinara huyo wa magaidi wa Daesh( IS) amedai kuwa mashambulio hayo yalitekelezwa na kundi lake kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha kushindwa wapiganaji wake katika kijiji cha Baghouz kilichoko mashariki mwa Syria.


Share:

Marekani yasisitiza kuendelea kuisaidia Saudia katika vita vyake dhidi ya Yemen

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ametetea msaada na ushirikiano wa nchi hiyo na Saudi Arabia katika vita vyake dhidi ya watu wa Yemen kwa kudai kuwa jambo hilo ni lenye maslahi makubwa kwa Marekani.

Mike Pompeo alitoa matamshi hayo jana Jumatatu akiashiria mashambulio ya makombora ya kulipiza kisasi yanayovurumishwa na harakati inayopendwa sana nchini Yemen ya Ansarullah, ambayo imekuwa ikitetea na kuilinda nchi hiyo kutokana na uvamizi wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia. 

Ansarullah imekuwa ikilenga na kuvishambulia vituo na taasisi muhimu za kistratijia za Saudia ili kuizuia nchi hiyo kuendeleza mashambulio yake hayo ya kivamizi dhidi ya taifa la Yemen. 

Marekani, Israel na Uingereza zimekuwa zikiipa msada mkubwa wa kijeshi Saudi Arabia na washirika wake tokea waivamie Yemen mwezi Machi mwaka 2015.
 
Msaada na ushirikiano huo wa Washington na Riyadh umekuwa ukikosolewa vikali ndani ya Marekani na hasa katika Kongresi ya nchi hiyo kufuatia kuuawa kinyama kwa Jamal Khashoggi, mwandishi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa kidhalimu wa Saudi Arabia, huko Istanbul Uturuki, mwezi Oktoba mwaka uliopita. 

Mapema mwezi huu, Rais Donald Trump wa Marekani alipinga kwa veto mswada uliopitishwa na Kongresi hiyo kwa ajili ya kusimamishwa ushirikiano na msaada huo wa kijeshi wa Marekani kwa Saudia.

Vita hivyo vimepelekea zaidi ya Wayemen 70,000 kupoteza maisha yao ambapo 10,000 kati yao waliuawa katika kipindi cha miezi mitano iliyopita. 

Vita hivyo pia vimeharibu pakubwa miundombinu ya nchi hiyo zikiwemo hospitali, shule, viwanda na barabara. Umoja wa Mataifa tayari umeonya kwamba Wayemen milioni 22.2 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na kwamba milioni 8.8 kati yao wanakabiliwa na hatari ya janga la njaa. Kwa mujibu wa ripoti ya umoja huo, Yemen inakabiliwa na janga kubwa zaidi la njaa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 100 iliyopita.


Share:

Wanajeshi 30 wa Nigeria watoweka kufuatia shambulizi la Boko Haram

Wanajeshi watano wa Nigeria wameuawa na wengine 30 kutoweka kufuatia shambulizi lililofanywa na magaidi wa Boko Haram katika kambi ya wanajeshi hao.

Katika shambulio lililofanywa na magaidi hao jana Jumatatu katika kambi ya wanajeshi hao huko katika mji wa Maiduguri, magaidi walifanikiwa kuiteka kikamilifu kambi hiyo. Kufikia sasa hakuna habari zozote zilizotolewa kuhusiana na hatima ya askari hao waliotoweka.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa kufuatia kuongezeka kwa duru mpya ya mashambulio ya magaidi wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 katika eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao na kuishi kama wakimbizi katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Katika mapigano ya miaka 9 ambayo yamekuwa yakiendeshwa kati ya magaidi hao na jeshi la Nigeria, zaidi ya watu elfu 27 wameuawa na wengine milioni moja na laki nane kuwachwa bila makazi na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.



Share:

Serikali Kuanzisha Mnada wa Kokoa Kyela

Serikali imesema itaanzisha mnada wa kuuza zao la kokoa linalozalishwa Kyela mkoani Mbeya.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa bungeni leo Aprili 30, amesema mkakati wa Serikali ni kutafuta wanunuzi wakubwa duniani kununua mazao kwenye mnada huo na kuachana na ule wa Mombasa nchini Kenya.

Awali Bashungwa pia ametoa onyo kwa baadhi ya wafanyabiashara wa pamba ambao wameanza kununua zao hilo kabla ya msimu kuanza Mei mwaka huu.

Akijibu swali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa kuhusu  nini kauli ya Serikali kwa wafanyabiashara walioanza kununua pamba kwa Sh 600 na 700.

Bashungwa amesema: “Anayenunua pamba kabla ya msimu kuanza rasmi ni kosa kisheria na atawasiliana na Wakuu wa Mikoa washughulikie suala hilo,”.


Share:

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne April 30




Share:

Monday, 29 April 2019

YANGA SC YAINYAMAZISHA AZAM FC YAICHAPA 1-0

YANGA SC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.

Shujaa wa Yanga SC leo ni mchezaji wake kipenzi cha mashabiki, Mrisho Khalfan Ngassa aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 13 akimalizia krosi nzuri ya kiungo mwenzake mshambuliaji, Ibrahim Ajibu Migomba.

Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 77 baada ya kucheza mechi 33 ikiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 69 za mechi 27, wakati Azam FC inabaki nafasi ya tatu na pointi zake 66 za mechi 33.

Yanga SC leo iliingia na maarifa ya kucheza kwa makini zaidi, ikijilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza, huku Azam FC wakionekana bora tangu mwanzo wa mchezo.

Na baada ya kupata bao lake hilo moja pekee la ushindi, Yanga SC ikazidisha mchezo wa kujihami na pamoja na Azam FC kuuteka mchezo na kushambulia zaidi, lakini hawakufanikiwa kupata bao.

Yanga ilipata pigo dakika ya 38 baada ya beki wake kushoto, Gardiel Michael kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, huku nafasi yake ikichukuliwa na Jaffar Mohammed. 

Kipindi cha pili, kocha wa Yanga SC, Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliimarisha safu ya ulinzi kwa kumtoa Ajibu na kumuingiza kiungo wa ulinzi, Said Juma ‘Makapu’.

Washambuliaji wa Azam FC, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Daniel Lyanga pamoja na kiungo Mudathir Yahya wote walikosa mabao ya wazi leo. 

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Nicolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Ennock Atta-Agyei dk76, Mudathir Yahya, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Gardiel Michael/Jaffar Mohammed dk38, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’, Heritier Makambo, Ibrahim Ajibu/Said Juma ‘Makapu’ dk76 na Raphael Daudi.
Share:

WAZIRI MKUU AZINDUA MAABARA YA TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi zinazofanya uhakiki na upimaji bidhaa nchini zijirekebishe na ziongeze kasi ya utoaji matokeo kwa wateja.


"Kumekuwa na malalamiko kutoka mipakani juu ya bidhaa zinazochukuliwa ili zikapimwe kwamba zinachukua muda mrefu. Punguzeni urasmi huo ili kufanya sekta ya biashara iweze kwenda kwa haraka zaidi. Tume yako (TAEC), TBS na TFDA ni miongoni mwa taasisi zinazolalamikiwa na wawekezaji na wafanyabiashara. Tumieni fursa hii kujirekebisha na kuharakisha utoaji wa matokeo," amesema.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Aprili 29, 2019) wakati akizindua maabara ya Maabara ya kisasa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission -TAEC) iliyopo Njiro, jijini Arusha.

“Nafahamu kuwa hii Tume inafanya kazi kwa karibu na bandari vituo vya mipakani ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Naamini kuanzia sasa mtaharakisha upimaji wa bidhaa na vifaa na kutoa majibu ya vipimo haraka,” amesema.

Waziri Mkuu ameitaka Bodi na Menejimenti ya Tume, waendelee kubuni na kuibua miradi mingine zaidi ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia. “Angalieni uwezekano wa kuanzisha kinu cha utafiti kinachotumia teknolojia ya nyuklia (Research Reactor); mtambo wa kuongeza thamani na ubora wa vitu mbalimbali ikiwemo matunda na mazao mbalimbali (multi-purpose irradiator); na mtambo wa kuzalisha dawa za kuchunguza na kutibu maradhi ya saratani (accelerator).”

Amesema kwa kufanya hivyo, maabara hiyo na watumishi wake wataongeza mchango wa teknolojia ya nyuklia kwenye ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Amesema anatambua kwamba Tume ya Nyuklia Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa wafanyakazi na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa maabara awamu ya pili. “Serikali inazichukua changamoto hizo na itaendelea na juhudi za kuzitafutia ufumbuzi kadiri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu,” amesema.

Waziri Mkuu ameishukuru Jumuiya ya Ulaya kwa msaada wa vifaa vya maabara hiyo vyenye thamani ya Euro milioni 2.2 (sawa na sh. bilioni 7.5) na kwamba Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Bodi na uongozi wa Tume hiyo wawapandishe vyeo watumishi watatu wa tume hiyo ambao aliwapa vyeti na zawadi ya sh. milioni moja kila mmoja kwa kukataa rushwa na kutokubali vitisho walivyopewa.

“Nimefurahi sana kuona watumishi watatu ambao ni wazalendo na wamekataa kupokea rushwa au kukubali vitisho walivyokuwa wakipewa na kuamua kusimamia misingi ya kazi zao. Hii zawadi mliyowapa haitoshi.”

“Watumishi hawa ni mfano wa kuigwa na wengine. Mwenyekiti wa Bodi waongeze fedha nyingine kila mmoja sh. milioni mbili ili jumla iwe milioni tatu na wapandishwe vyeo huko waliko ili iwe motisha zaidi kwao. Sijui muundo wenu ukoje, lakini nataka nipate taarifa ya utekelezaji wa haya maamuzi kesho kutwa, baada ya Mei mosi,” amesisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu awape vyeti na zawadi, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Najat Mohamed aliwataja watumishi hao kuwa ni Machibya Matulanya wa kituo cha Mtwara na mpaka wa Kilambo (Tanzania) na Msumbiji; Patrick Simpokolwe na Geofrey Kalolo wa kituo cha Tunduma (Tanzania) na Zambia.

Machibya Matulanya ambaye cheo chake ni mtafiti wa mionzi daraja la pili (Radiation Health Physics Research Officer II) amekuwa akitegewa mitego ya rushwa na kupokea vitisho kutoka wa wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.

Patrick Simpokolwe ambaye cheo chake ni mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili (Radiation Safety Inspector II) na Geofrey Kalolo ambaye ni mtumishi wa kujitolea (volunteer) naye pia anafanya kazi kama mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili. Wote kwa pamoja walipokea vitisho walipozuia mzigo kutoka Zambia wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 usiingizwe nchini.

(mwisho).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,


Share:

Mfumo Wa Taifa Wa Takwimu Za Mtakuwwa Kusaidia Kupunguza Ukatili Dhidi Ya Wanawake Na Watoto

NA: MWANDISHI WETU
Mfumo wa Taifa wa takwimu za MTAKUWWA utasaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Asanterabi Sang’enoi wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali kutoka  kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mashirika ya Kimataifa na Asasi za Kiraia kujadili mfumo na nyenzo kwa ajili ya udhibiti wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto utakaohusisha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, kutoa taarifa na ufuatiliaji kilichofanyika katika ukumbi wa Umwema uliopo Mkoani Morogoro.

Alieleza kuwa lengo la mpango kazi huo ni kuboresha mifumo itakayo saidia kuwa na taarifa na uwepo wa takwimu sahihi ambazo zitasaidia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa asilimia 50 ifikapo 2022.

“Uwepo wa mfumo huo utawezesha wadau kupata uelewa juu ya ukusanyaji wa taarifa na takwimu kwa kuandaa taarifa ambazo zitasaidia kupima maendeleo ya Mpango Kazi wa Kudhibiti Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto hapa nchini,” alisema Sang’enoi.

Aidha aliwataka wadau wa kikao kazi hiko kushirikiana kwa pamoja ili waweze kuwa na mifumo ya taarifa sahihi na takwimu rasmi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Mathias Haule alieleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto barani Afrika kwa na inaongoza kwa kuwa na mifumo mingi ya ulinzi kwa wanawake na watoto ikiwemo uanzishwaji wa madawati ya jinsia na watoto.

Naye, Bi. Lucy Tesha kutoka UN Women alisema kuwa alisema kuwa kikao kazi hiko kitamwezesha kila mdau kutambaua majukumu yake na kuweza kukusanya taarifa kwa kutumia mfumo mmoja ambao utakuwa na data sawia ambazo zitakuwa hazijirudi kama ilivyokuwa awali.

Pia, Mchumi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni Mratibu wa Madawati ya Jinsia na Watoto Bi. Happiness Mugyabusi alifafanua kuwa mpango kazi utasaidia kuwa na takwimu za awali ambazo zitawezesha kutambua ndani ya miaka mitano ijayo Taifa lilivyopiga hatua katika kutatua masuala haya ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Nchi yetu ina programu nyingi zinazozingatia udhibiti wa ukatili dhidi ya wanawake na watoto lakini wadau wameshindwa kuratibiwa vizuri kwa kukosa mfumo sahihi wa kukusanya taarifa na hivyo kupelekea kuwaleta wadau kwa pamoja ili kuwa na taarifa na takwimu za pamoja na uratibu mzuri wa wadau wote wa masuala ya wanawake na watoto,” alisema Mugyabusi.

Katika kikao kazi hiko wadau mbalimbali waliweza kushiriki ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu ambao ndio waratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, MUHAS, Mashirika ya Kimataifa (UN – Women), Asasi za Kiraia ( Child Watch, WFT, TCRF, WILDAF, TGNP na TECDEN).


Share:

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini Afanya Mabadiliko ya Baadhi ya Makamanda wa Mikoa




Share:

IMF: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vinavuruga ukuaji wa uchumi katika eneo la Mashariki ya Kati

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema leo kwamba vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, kuongezeka kwa machafuko katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na tatizo la bei ya mafuta vinadhoofisha ukuaji wa kiuchumi katika kanda hiyo. 

Mkurugenzi wa IMF wa Idara ya Mashariki ya Kati na ya Asia ya Kati, Jihad Azour, amesema hali hiyo pia inachochea ukosefu wa ajira katika kanda hiyo. 

"Kasi ya polepole ya ukuaji wa uchumi inazua kutengenezwa ajira zinazohitajika ambazo zitawawezesha kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira. Katika miaka mitano ijayo, kanda hiyo inahitaji kuunda nafasi mpya za kazi zaidi ya milioni 25, ili kuimarisha kiwango cha ukosefu wa ajira kinachoshuhudiwa sasa katika kiwango cha juu," amesema Jihad Azour. 

Shirika hilo linatabiri uchumi wa Iran, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika kanda hiyo baada ya Saudi Arabia, utaanguka kwa asilimia 6.0 mwaka huu baada ya kupungua kwa asilimia 3.9 mwaka 2018. 

Uchumi wa Iran umeanza kuporomoka baada ya Marekani kuamua kuiwekea tena vikwazo nchi hiyo, kufuatia Rais Donald Trump kujitoa katika makubaliano ya silaha za nyuklia ya mwaka 2015.


Share:

Majeshi ya majini ya Iran na Urusi kufanya mazoezi Ghuba ya Uajemi

Majeshi ya majini ya Iran na Urusi yanapanga mazoezi ya pamoja na ya kipekee katika Ghuba ya Uajemi baadaye mwaka huu.

Hayo yametangazwa na Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Admeri Hossein Khanzadi ambaye ameyadokeza hayo alipozungumza na waandishi habari mapema leo  mjini Tehran baada ya kurejea kutoka China ambapo amekutana na makamanda wenzake kutoka kote duniani.

Admeri Khanzadi ameongeza kuwa, tayari mazungumzo yameshaanza na Urusi  kuhushu maozeozi hayo ya pamoja.

Majeshi ya majini ya Iran na Urusi  hufanya mazoezi ya pamoja mara kwa mara katika Bahari ya Kaspi na kwa msingi huo mazoezi yajayo katika Ghuba ya Uajemi yatainua kiwango cha uhusiano wa pande mbili.
 
Admeri Khanzadi aidha ameashiria mpango wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuimarisha uhusiano wa mafunzo na majeshi ya majini ya nchi zingine na kusema: "Iran inachunguza mwaliko kutoka nchi kama vile India, China, Pakistan na Italia ambazo zimetaka ushirikiano katika mafunzo kwa maafisa wa kijeshi."

Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye alitishia kuzishambulia meli za mafuta za Iran na kusema "maji ya kimataifa ni ya nchi zote, na hivyo jeshi la majini lina jukumu la kulinda maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran." 

Admeri Khanzadi amesisitiza kuwa, meli za mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni sehemu ya ardhi ya nchi hii na zitalindwa kikamilifu.


Share:

Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya elimu ya Juu Yashauriwa kuweka fedha za wanafunzi moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendelo ya Jamii, imeishauri Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya elimu ya Juu (HESLB) kuweka fedha za kujikimu za wanafunzi moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi ili kuepuka changamoto zinazojitokeza.

Akisoma hotuba ya Kamati hiyo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, bungeni leo Aprili 29, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Nkamia amesema wanafunzi wamekuwa wakichelewa kupata fedha za kujikimu kutokana na changamoto mbalimbali zinazokabili vyuo vyao na baadhi ya benki nchini.

Amesema kutokana na baadhi ya vyuo kuwa na madeni ya mikopo benki, fedha za kujikimu za wanafunzi  zimekuwa zikizuiwa na hivyo kusababisha hali ngumu kwa wanafunzi.

Nkamia ambaye pia ni Mbunge wa Chemba,(CCM) amesema Kamati imeshauri serikali kuhakikisha inaboresha maslahi ya wahadhili na watumishi wa vyuo vikuu, hususani posho ya nyumba ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.


Share:

POLISI KUKAMATA WANAOTEMBEA WAMELEWA POMBE MTAANI

Polisi nchini Uganda inapania kuzindua mpango wa kuwakamata watembea kwa miguu watakaopatikana wakiwa walevi.

Akitetea mpango huo mpya kamanda wa trafiki katika jiji la Kampala Lawrence Niwabiine amesema kikosi cha polisi hakitaruhusu watu "wahatarishe"maisha yao.

Tayari vyombo vya habari nchini Uganda vimezua gumzo mitandaoni baada ya kuangazia mpango huo tata katika mitandao ya kijamii.

Watu wamekua wakihoji jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu wanaokamatwa kila uchao wakiendesha magari wakiwa walevi huishia kuachiwa katika mazingira ya kutatanisha.

Hata hivyo kuna mamia ya watu waliyopatikana na hatia ya kuendesha magari wakiwa walevi wameshindwa kulipa faini.
Hatua hii imepokelewaje?

Gazeti la New Vision limeendeleza gumzo hilo katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuelezea sheria hiyo inayopendekeza kuwa mtu akipatikana na hatia atapigwa faini ya hadi dola 10,000 na pia kuwauliza wasomaji wake kutoa maoni kuhusiana na pendekezo hilo.

Kuna wale wanaosema kwa kuwa Afande Niwabiine hatumii kileo huenda maafiasa wake wakawatia mbaroni walevi wanaotembea kwa miguu kando ya barabara.

Wengine wanasema hatua hiyo huenda ikawa na athari kwa uchumi wa nchi.

Wanaharakati wanapendekeza mifumu ya kisheria na kijamii iwekwe sawa kabla ya kuanza kutekeleza sheria hiyo.

''Kabla ya kuanza mpango huo,magereza yatahitaji kupanuliwa haraka iwezekanavyo kwasababu watembezi wengi walevi hawana uwezo wa kulipa faini la sivyo mahakimu watakuwa na kibarua kigumu katika kutoa hukumu dhidi ya watu hao wakati sheria inasem kila mmoja achukukliwe hatua'' alisema mmoja wao.

Pili anasema wafanyibiashara wa pombe watalazimika kuhamisha biashara zao katika maeneo ya makazi ili kupunguza hofu ya wateja wao kukamatwa.

''Hata polisi akipiga kambi karibu na hapo akisubiri kukukamata hataweza kufanya hivyo manake unaweza kuamua kumpigia mmoja wa jamaa zako nyumbani kukuletea mtu ulale ndani ya baa karibu na kwako'' ,aliongeza.

Pia anasema kumbi za burudani zitapoteza umuhimu kwasababu kile ninachowavutia wateja ni pombe

Wafanyibiashara wa texi wapokea vyema pendkezo hilo kwasababu walevi watalazimika kutumia huduma zao za usafiri kwa kuhofia kukamatwa.

Baadhi ya wakaazi wamewaonya wenzo wanaopenda kubugia pombe kuwa makini hata wanapotumia usafiri wa umma kwasababu polisi huenda wakawasubiri katika stendi ya mwisho wa gari.
Chanzo - BBC
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger