Na. Catherine Sungura,WAMJW-Mwanza
Katika vita dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza Taaluma ya Famasi ni muhimu katika kuwezesha upatikananji wa bidhaa za dawa kwa wale watakaoshindwa kuzuia kupata magonjwa yasiayoambukiza na ikawalazimu wafike vituoni kupata tiba.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa Kongamano la 12 la kisayansi la Chama cha Wanafunzi wa Taaluma ya Famasi (TAPSA) lililofanyika jijini Mwanza.
Dkt. Gwajima amebainisha kwamba bidhaa hizo za dawa kwa ajili ya kundi hilo ni ghali na bahati mbaya nchini Tanzania hakuna kiwanda cha kutengeneza na badala yake wanaagiza toka nje ya nchi.“Tunapaswa kutafakari iwapo kasi ya kukua kwa maradhi haya ni inaongezeka je tunazijazititi vipi kwenye kasi ya kinga kwani bado kasi hiyo ni ndogo”.Aliongeza Dkt. Gwajima.
Alisema kuwa, katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora karibu zaidi na wananchi kwa kujenga miundombinu , kuajiri watumishi na kuweka vifaa tiba na dawa. Maboresho haya yameendelea kufanyika katika vituo vya huduma za afya ngazi zote.
Hata hivyo amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo changamoto ya upatikanaji wa bidhaa za dawa na vifaa tiba kwa ajili ya huduma mbalimbali zikiwemo na huduma kwa ajili ya wanaougua magonjwa hayo yasiyoambukizwa.
Aidha, Dkt. Gwajima amesema wapo baadhi ya wanataaluma wachache wasio waadilifu na wasio wazalendo ambao ni doa kubwa kwenye taaluma hiyo adimu ambayo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye ajenda ya afya. Hivyo iwapo itasimama kwa nafasi yake basi wanataaluma hao wanaweza kufanya mapinduzi makubwa ya afya na kiuchumi.
“hii itawezekana kwa kujikita kwenye ajenda ya jinsi gani viwanda vya ndani viweze kuzalisha bidhaa mbalimbali na kuhakikisha matumizi yasiyotia shaka ya bidhaa za afya zinazopokelewa kwenye vituo vya huduma na kuepuka upotevu na matumizi yasiyofuata miongozo na kusababisha usugu wa baadhi ya dawa na pia baadhi kuleta madhara kwa wateja kama ilivyokusudiwa”.
Dkt. Gwajima alitoa rai kwa jamii ya kitanzania kuzingatia ulaji unaofaa ambapo kila mlo uwe na makundi yote matano ya vyakula halisi, kutotumia mafuta mengi,chumvi nyingi,kufanya mazoezi ,kupata usingizi wa kutosha,kuepuka matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya na pia kuchunguza afya angalau mara moja kwa mwaka.
Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinavyohusu watu wenye miaka 30 hadi 70 husababishwa na magonjwa hayo.Hapa nchini inakadiriwa kuwa magonjwa yasiyoambikiza husababisha asilimia 27 ya vifo vyote.Kauli mbiu ya Kongamano hilo mwaka huu ni “Wataalamu wa Famasi: kuongeza wigo katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza”.
Awali akiongea wakati wa kongamano hilo Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi aliwataka wafamasia na wataalum wengine wa afya nchini kuhakikisha wanatumia fomu za dawa( prescription form) kama nyenzo muhimu za kuondoa changamoto za dawa kwani dawa ni fedha za haraka hivyo wahakikishe kabla hawajatoka lazima wahakikishe dawa zinatoka kwa kujaza fomu hizo.
Aliongeza kuwa kwenye kutenda kazi za umma lazima wafuate miongozo ikiwemo muongozo wa matibabu nchini (STG) wanapokuwa sehemu za kazi hivyo ni wakati wao sasa wa kupitia na kuelewa nini wanapaswa kutekeleza kwenye kazi zao.
Hata hivyo Bw. Msasi aliwataka chama hicho kuanziasha klabu za mazoezi kwenye vyuo vyao ili kuweza kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa vitendo na hiyo itasaidia jamii kuelewa umuhimu wa kufanya mazoezi.
Naye Mlezi wa wanafunzi wa Famasi na Masajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth shekalaghe aliwataka wanafunzi hao kufanya kazi kwa kujitoa, kuwajibika na kuipenda taaluma yao ili kuweza kuitumikia vyema taaluma yao.
Bi. Shekalaghe alisema kama Baraza wataendelea kusimamia na kuhakikisha wanaendeleza taaluma kwa kutoa elimu ya maadili kwenye vyuo vya famasi nchini ili wanapokua chuoni wazitambua na kuzijua angali wanafunzi.
Naye Rais wa Chama cha Wafamasia Wanafunzi Tanzania(TAPSA) Bw. Hamis Msagama ameipongeza Serikali kwa uboreshaji wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi kubwa inafanywa na wafamasia na kuonesha jinsi gani inawajali watanzania.
Pia Bw.Msagama ameipongeza Wizara ya Afya kwa kuanzisha kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD) hivyo wao kama chama waliona ni vyema kongamaono lao mwaka huu kujadili kwa kina namna ya kupambana na magonjwa hayo ambayo yanaathiri watu wengi nchini na duniani.
0 comments:
Post a Comment