Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewataka wanasiasa na wagombea wanaodai kuwepo kwa vituo na wapigakura hewa kupeleka ushahidi na endapo wakishindwa kufanya hivyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Dk.Wilson Charles amesema tuhuma hizo zinaleta kuzua taharuki kwa jambo ambalo si la kweli.
Aidha, amesema vituo vya kupigia kura ni vingi kuliko vya kujiandikishia kwa sababu kila kituo wameweka idadi ya wapigakura wasiopungua 500 ili kurahisisha zoezi la upigaji kura.
"Vituo vilivyotumika kuandikisha wapiga kura vilikuwa 37,814,na vituo vya kupigia kura ni 80,155, hii inatokana na kwamba kwenye kituo kimoja kilichotumika kujiandikisha kinaweza kutoa vituo vitatu kwa sababu kituo kimoja kinatakiwa kuwa na wapiga kura 450 hadi 500," amesema
Amewataka wagombea wa kiti cha uais na Makamu wa Rais kuzingatia ratiba toleo la sita ya kampeni iliyotolewa na Tume.
Mkurugenzi huyo, amesema Tume imejiandaa vizuri katika uchaguzi huo na kwamba tayari vifaa vyote muhimu leo vitakuwa vimefika kwenye majimbo ya Tanzania bara na Zanzibar.
"Pia Tume inawataka wasimamizi wa majimbo wafikishe kuanzia leo vifaa kwenye vituo vya kupigia kura ili kusijitokeze dosari zozote kwenye uchaguzi ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na kufunguliwa vituo," amesema.
0 comments:
Post a Comment