Sunday, 30 August 2020

VIGOGO YANGA SC YAWACHAPA AIGLE NOIR 2-0 KILELE CHA WIKI YA MWANANCHI

...

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Vigogo wa soka Tanzania, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa wa Burundi, Aigle Noir katika mchezo wa kirafiki usiku wa leo Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.

Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais mstaafu wa awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete – Aigle Noir iliwaruhusu Yanga kupata mabao baada ya kiungo wake, Mghana Koffi Kouassi kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 29 kufuatia kuonyeshwa kadi ya njano ya pili na refa Martin Saanya wa Morogoro. 

Baada ya hapo Yanga SC wakapata bao la kwanza dakika ya 39 likifungwa na winga wake mpya, Tuisila Kisinda aliyemchambua kipa Mtanzania wa Aigle Noir, Erick Johola kufuatia pasi nzuri ya Feisal Salum ‘Fei Toto’. 

Mshambulaji mpya, Mghana Michael Sarpong akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 59 kwa kichwa kikali kutoka umbali wa mita sita kufuatia krosi maridhawa ya Ditram Nchimbi.

Na ikashuhudiwa kipindi cha pili kocha mpya wa Yanga SC, Mserbia Zlatko Krmpotic akibadili kikosi kizima.

Mchezo huo ulitanguliwa na burudani ya muziki iliyoongozwa na msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ aliyeingia uwanjani kwa kushuka na kamba mithili ya Komandoo.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata/Farouk Shikhalo dk60, Kibwana Shomari/Paul Godfrey ‘Boxer’ dk81, Yassin Mustafa/Adeyoum Ahmed dk67, Abdallah Shaibu ‘Ninja’/Carlos Carlinhos dk81, Bakari Mwamnyeto/Said Juma ‘Makapu’ dk67, Mukoko Tonombe/Zawadi Mauya dk54, Tuisila Kisinda/Waziri Junior dk54, Feisal Salum ‘Fei Toto’/Haruna Niyonzima dk54, Michael Sarpong/Abdulaziz Makame dk67, Ditram Nchimbi/Farid Mussa dk54 na Deus Kaseke/Juma Mahadhi dk67.

Aigle Noir; Erick Johola, Ndikumana Desire, Hitimana Hamza, Yanick Nkurunziza, Masoud Marcsse, Koffi Kouassi, Ndikumana Asman, Ngabonziza Blanchare, Christ Attegbe na Nzojibwami Frank.

CHANZO- BINZUBEIRY BLOG
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger