Thursday, 2 April 2020

Waziri Wa Kilimo Na Waziri Wa Viwanda Waongoza Kikao Kazi Kujadili Ufungamanishaji Wa Sekta Ya Kilimo Na Mikakati Ya Kutafuta Masoko

...
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kadhalika, Wizara ya Viwanda na Bishara, na Taasisi za soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Taasisi ya kuendeleza Kilimo Afrika (AGRA) wamekutana Jijini Dodoma kujadili kwa pamoja namna ambavyo Wizara hizo mbili zinaweza kuongeza mshikamano na weledi wa kiutendaji kwa ajili ya kufungamanisha uchumi wa Kilimo na Viwanda.

Katika kikao hicho kilichotuama katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo maarufu kama Kilimo IV kikiongoza na mawaziri kutoka pande mbili, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Waziri wa Viwanda na Bishara Mhe Innocent Nashungwa (Mb) kwa pamoja wamesisitiza ulazima wa wataalamu hao kuunganisha nguvu kwa pamoja baina ya Wizara na Taasisi za umma na binafsi ili kuimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu Uzalishaji, uhifadhi, Ubora kwa Mazao ya kimkakati na mchanganyiko.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Kilimo Mhe Japhet hasunga (Mb) amewataka Wataalamu hao kuimarisha intelijensia ya masoko kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo na ufuatiliaji wa karibu wa mwenendo wa masoko ya Mazao na bidhaa ulimwenguni.

Hasunga amesema kuwa  pamoja na mikakati ya masoko lakini wataalamu hao wanaweza kujadili na kuona namna ya kuimarisha uhifadhi wa Mazao ya wakulima baada ya kuvuna kwani Barani Afrika nafaka myingi hupotea mara baada ya kuvuna.

Amewataka wataalamu hao pamoja na mambo mengine amewataka kuhakikisha kuwa wanaimarisha miundombinu ya masoko ikiwemo maghala ya kisasa ya kuhifadhia Mazao na bidhaa.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Innocent Bashungwa (Mb) amesema kuwa intelijensia ya masoko inapaswa kuhakikisha kwa haraka inatumia Balozi za Tanzania nje ya nchi katika kutafuta fursa za masoko ya Mazao  na bidhaa pamoja na kuanzisha madawati ya biashara (Trade/Commercial attache) Kwenye balozi hizo.

Pia amesema mpango mkakati wa kuwaunganisha wakulima na wasindikaji ndani na nje ya nchi ni muhimu kutekeleza haraka iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo zaidi katika kuongeza Uzalishaji wenye tija ili kukidhi nahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. 

Kadhalika Waziri Bashungwa ameongeza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) wanapaswa kukutana na Shirika la Chakula Duniani (WFP) kujadili uimarishaji wa masoko ya Mazao mbalimbali.

Pamoja na mambo mengine Waziri Bashungwa ameitaka Taasisi ya kuendeleza Kilimo Barani Afrika (AGRA) kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya Kilimo ili kutafuta ufunguzi wa namna ya kuimarisha masoko ya Mazao ya wakulima nchini.

MWISHO



Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger