Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshangazwa na uwezo wa mwanafunzi wa kidato cha kwanza asiye na mikono anayetumia miguu kuandika na kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi nchini kuwafichua wazazi na walezi wanaowaficha watoto wenye mahitaji maalumu.
Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati alipozindua shule jumuishi ya watoto walemavu ya Mtakatifu Pamakio inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi iliyopo Hai, mkoani Kilimanjaro.
Akiwa shuleni hapo alikutana na mwanafunzi huyo Joseph Mtei ambaye hana mikono yote na kushangazwa na jinsi anavyotumia mguu wake wa kulia kuandika.
“Nimeshuhudia maajabu ya Mungu kumwona mtoto huyu akiandika mwandiko mzuri unaosomeka zaidi ya hata wale ambao wana mikono miwili,” alisema Majaliwa.
Alitoa wito kwa wazazi wote nchini kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu na kuhakikisha wanaenda shule kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine.
“Viongozi wote wa mikoa hakikisheni watoto wote wenye ulemavu wanaenda shule, hakuna sababu ya kumweka mtoto mwenye mahitaji maalumu nyumbani, wote waende shule wapate elimu sawa na wengine,” alisema Majaliwa.
Pia aliziagiza taasisi zote za umma kuhakikisha wanatembelea shule zenye Watoto wenye mahitaji maalum ili kubaini changamoto wanazokumbana nazo ili serikali pamoja na wadau wengine waweze kuwasaidia.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema kusiwe kikwazo kwa watoto wenye ulemavu na kwamba wanapaswa kupata elimu sawasawa na watoto wengine.
“Nimpongeze Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Arusha, Askofu Isaac Amani kwa kutambua umuhimu wa haki za watoto wenye ulemavu wa kupata elimu kwa kuwa na wazo zuri la kuhakikisha watoto hawa wanapata elimu,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu shule hiyo, Askofu Amani alisema lengo la kuianzisha ni kuhakikisha watoto wenye uhitaji maalumu waliotelekezwa na waliosahaulika na jamii wanapata fursa ya elimu.
Mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi aliyekuwapo katika ziara ziara hiyo alisema hataacha kuwasaidia watoto wenye ulemavu kwani ni sehemu ya maisha yake.
“Nitaendelea kuwa na watoto hawa wenye uhitaji maalumu hadi Mungu atakaponichukua duniani maana watoto hawa wamekua ni sehemu ya maisha yangu na nawapenda sana na leo hii naipa shule hii Sh1 bilioni kwa ajili ya kuhakikisha watoto hawa wanapata mahitaji muhimu,” alisema Mengi.
0 comments:
Post a Comment