Saturday, 26 January 2019

SHULE YASHANGAA KUSHIKA MKIA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE

...

 
Shule za sekondari Kwizu na Masjadi Qubah zilizo miongoni mwa 10 zilizofanya vibaya kitaifa mtihani wa kidato cha nne 2018, zimetaja sababu ya kutofaulisha vizuri, huku mkuu wa shule ya Kwizu, Peter Mngulwi akisema matokeo yamewashangaza kwa kuwa wanafunzi wao walijiandaa vizuri.

Mbali ya shule hizo, zingine zilizofanya vibaya kitaifa ni Pwani Mchangani (Kaskazini Unguja), Ukutini (Kusini Pemba), Kwediboma (Tanga), Rwemondo (Kagera), Namatula (Lindi), Kijini (Kaskazini Unguja), Komkalakala (Tanga) na Seuta (Tanga).

Wakati Masjadi Qubah na Mkwizu zikitoa ufafanuzi wa matokeo mabaya waliyoyapata, askari PC Hamisi wa Kituo cha Polisi Malinyi anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu wa mitihani hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa aliliambia Mwananchi jana kuwa, askari huyo alishiriki kufanya udanganyifu huo wakati akisimamia mtihani katika Sekondari ya Tumaini Lutheran iliyopo wilayani humo.

Tuhuma za askari kujihusisha na udanganyifu zilitajwa pia juzi na katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde katika mkutano wake na wanahabari wakati akitangaza matokeo hayo.

Dk Msonde alisema walibaini udanganyifu uliohusisha utoboaji wa tundu katika ukuta ambapo mitihani hiyo ilikuwa ikipitishwa kwenda kwa walimu kupitia kwa wanafunzi wa kidato cha pili ili wakaifanye na kisha ilirejeshwa katika chumba cha mtihani na askari.

Katika matokeo hayo, Masjadi Qubah ndio imeshika mkia kitaifa huku Kwizu ikiwa ya tatu kutoka mkiani.

Akizungumzia matokeo hayo jana, mwalimu mkuu wa Sekondari ya Kwiuzu, Mngulwi alisema yamewachanganya na hawakuyatarajia.

“Matokeo yametuchanganya hatujui nini kimetokea. Wanafunzi walijiandaa vizuri sana na tulitarajia matokeo mazuri, nashindwa kuelewa shida ni nini. Niko kwenye state of shock (hali ya mshtuko),” alisema Mngulwi.

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger