Wanafunzi
wa kidato cha pili nchini wameanza kufanya mitihani yao ya upimaji leo
katika shule za sekondari 4,669 zilizopo Tanzania Bara.
Jumla ya wanafunzi 435,221 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo wakiwamo 67 wasioona na 306 wenye uoni hafifu.
Mbali
na mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta), Dk Charles Msonde amesema mtihani wa Taifa wa darasa la nne
utafanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu.
"Mitihani
hii inafanyika katikati ya mafunzo ili kubaini changamoto zilizopo na
kutafuta namna ya kuboresha mafunzo hayo," amesema Dk
Msonde.
Wakati
huo huo, Dk Msonde amefafanua kuwa mafunzo ya ualimu wa shule ya msingi
ngazi ya stashahada yamefutwa lakini wanafunzi waliopo vyuoni
watamalizia masomo yao kwa muda uliobaki.
Dk Msonde amesema mafunzo hayo ya walimu yataendelea kwa utaratibu wa zamani ambao ulikuwa ngazi ya cheti.
Amesema usimamizi wa mitihani hiyo itakuwa chini ya Necta kama ilivyokuwa zamani badala ya Nacte.
"Wanafunzi
walio vyuoni wataendelea na mafunzo hayo, isipokuwa kuanzia mwaka huu
hatutadahili kwa ngazi ya diploma, tutadahili ngazi ya cheti kama
ilivyokuwa zamani," amesema Dk Msonde.
0 comments:
Post a Comment