Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma limesambaratisha mahafali ya wanachama wa umoja wa wanafunzi wa Chadema vyuo vikuu (Chadema Students Organization -CHASO ) yaliyokuwa yanafanyika katika Ukumbi wa African Dreams ulipo Area D mjini Dodoma kwa madai kuwa ni utekelezaji wa agizo la kuzuia mikusanyiko ya vyama vya siasa kufuatia kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani.
Katika hafla hiyo mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambapo baadhi ya wanafunzi wamekamatwa baada ya kuambiwa watawanyike.
Polisi wamesema mikusanyiko yote ya kisiasa ilishapigwa marufuku, hivyo hata mahafali hiyo ilikuwa batili.
Mahafali hayo ambayo mapema yalitanguliwa na zoezi la uchangiaji damu ambapo wanafunzi walishiriki kikamilifu zoezi hilo kabla ya afisa mmoja wa Jeshi la Polisi kuingia katika ukumbi wa mahafali na kuhoji uhalali wake , hali iliyozua sintofahamu kabla ya magari ya polisi likiwemo lile la maji ya kuwasha kuingia katika eneo hilo na askari kutanda kila kona.
Mara baada ya askari hao kutapakaa yakaibuka malumbano makubwa kati ya maofisa wa Jeshi la Polisi na baadhi ya vingozi wa Chadema na wabunge wakiongozwa na Naibu katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar Salum Mwalimu huku wakiwaamuru polisi kuondoka eneo hilo na kuwataka vijana kuendelea na shughuli ya mahafali.
Baada ya malumbano hayo baadhi ya maofisa wa Polisi walionekana kuitana pembeni kwa ajili ya kuteta jambo na punde likasikika tangazo la kuwataka watu wote walioko katika eneo hilo kusambaratika huku pia wakipiga marufuku mikusanyiko na matembezi yanayoashiria maandamano.
Baada ya kusambaratishwa kwa mahafali hayo mwandishi wa habari hizi alizungumza na baadhi ya washiriki ambao ni wanachama wa CHASO ambapo wamesema kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi kinaonyesha namna gani serikali inavyokandamiza Demokrasia.
Edward Simbeye ni Katibu Mwenezi wa vijana Chadema Taifa ambaye pia ndiyo mratibu wa shughuli hiyo ya mahafali amesema hali hiyo ikiachwa iendelee ipo siku wananchi watakosa uvumilivu na kujichukulia maamuzi ambayo yatahatarisha amani ya nchi.
0 comments:
Post a Comment