Wednesday, 2 July 2014

CHADEMA YAFUNGUKA:OFISI YA MSAJILI WA VYMA VYA SIASA INATUMIWA

...
INNOCENT-THE BLOGGER-BOY
mnyika_d2c6c.jpg
Dar es Salaam. Mvutano mpya umeibuka baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumvaa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kikidai ofisi yake inatumiwa na wasaliti wa chama hicho.
Pia, chama hicho kimemtaka Jaji Mutungi ajitokeze hadharani kubainisha iwapo yeye ndiye aliyemtuma msaidizi wake, Sistyl Nyahoza kutangaza kuwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa hawana sifa ya kugombea uongozi ndani ya chama hicho kutokana na kuzuiwa na katiba ya Chadema.

Jana, Nyahoza alikaririwa na vyombo vya habari akisema Mbowe na Dk Slaa hawana sifa za kugombea uongozi wa chama hicho kutokana na katiba ya chama chao kuwabana.
Alibanisha kuwa kipengele cha ukomo wa mgombea katika katiba yao ya mwaka 2006 kiliondolewa kinyemela bila idhini ya mkutano mkuu.
Nyahoza alisema katiba ya Chadema ya mwaka 2004, ilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka kuwa kiongozi aliyeongoza vipindi viwili vya miaka mitano mitano, hawezi kuwania tena nafasi hiyo.
Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema Jaji Mutungi hana mamlaka ya kubaini sifa za viongozi wa chama hicho, bali wenye mamlaka hayo ni wanachama wa chama hicho pekee.
Mnyika alisema mwaka 2006, katiba ya Chadema haikurekebishwa, bali iliundwa upya na kuridhiwa na mkutano mkuu wa chama na kwamba Agosti 13, 2006 ilizinduliwa na nyaraka zote alikabidhiwa Msajili wa Vyama wa wakati huo, John Tendwa.
Katika uzinduzi huo wa katiba pamoja na bendera mpya ya Chadema, Tendwa alikimwagia sifa chama hicho kwa kuonyesha mwelekeo na mwenendo mzuri na kuvishauri vyama vingine viungane nacho kuunda chama cha upinzani chenye nguvu nchini.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Mbowe alikaririwa na gazeti hili Agosti 15, 2013 akisema yalikuwa yanalenga kuimarisha mapambano ya kisiasa ya chama hicho.
Mnyika alisema: "Mkutano mkuu wa chama uliipitisha Katiba hiyo baada ya mchakato mrefu wa kukusanya maoni kutoka kwa mabaraza ya wilaya na majimbo. Hatukurekebisha katiba kama inavyoidaiwa. Ni makubaliano ya wanachama wote ambao waliafikiana na mambo yaliyotakiwa kuwamo."
Alisema katika mchakato huo kulikuwa na makubaliano na mabishano katika baadhi ya masuala lakini suala la ukomo wa uongozi liliafikiwa na wanachama wote bila tatizo na kupitishwa kuingia katika katiba na Ofisi ya Msajili ilipelekewa fomu ya marekebisho pamoja na katiba mpya kama sheria inavyotaka... "Kama wameipoteza waseme tuwapatie katiba wairejee."
"Tunachomtaka Mutungi ni kuheshimu katiba ya chama na kuwaheshimu wanachama wa Chadema na ayapuuze madai ya wasaliti wachache. Kama vipi asubiri aone uamuzi wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu ubainishe kama katiba ilivunjwa," alisema Mnyika.
Mnyika alisema wameshtushwa na kauli ya ofisi hiyo na kuituhumu kwamba imeanza kutumika kisiasa na wasaliti.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa suala hilo jana, Jaji Mtungi alisema: "Hili suala lisimamiwe na chama husika kwa kuwasiliana na Ofisi ya Msajili... hakuna haja ya kulikuza katika vyombo vya habari. Wanachama wa Chadema watapata taarifa kutoka kwa viongozi wao ni nini kinaendelea."
Kuhusu madai kwamba ofisi yake inatumika kisiasa alisema: "Kama nilivyosema, hayo tuyaache hii ofisi yetu ipo more technical (kitaalamu zaidi) hatuingizi siasa. Wao (Chadema) waje kwenye ofisi yetu tuongee kama taasisi, iwapo tunataka kuwasilisha jambo katika vyombo vya habari, basi tutaitisha mkutano na waandishi wa habari," alisema Mutungi.
Mamlaka ya msajili
Mnyika aligusia pia mamlaka ya msajili huyo akisema... "Hana mamlaka ya kutangaza sifa za mgombea wa Chadema. Sifa na uamuzi vimetajwa katika katiba na kanuni za chama. Kifungu cha 6.3.2 cha katiba ya 2006 kinabainisha wazi kuwa kiongozi aliyemaliza muda wake na mwenye sifa ya kugombea anaruhusiwa kugombea...?" Alisema hata katika uchaguzi wa ndani wa mwaka 2009 viongozi wengi walichaguliwa na wakiwa wameshamaliza ukomo wa uongozi na msajili wa vyama hakuzungumza chochote.
Alisema hawababaishwi wala kuguswa na uamuzi uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa kwa kuwa mkutano mkuu wa Chadema unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ndiyo utakaoamua hatima wa kiongozi yeyote wa chama hicho
Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger