Friday 19 July 2024

MAGAZETI YA LEO JUMAMOSI JULAI 20, 2024

Share:

WAZIRI JAFO AKAGUA UJENZI WA JENGO LA OFISI ZA TBS JIJINI DODOMA


WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo,akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.

Na Gideon Gregory -DODOMA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ametoa maagizo kwa Taasisi zake zote kutumia bidhaa za ndani za ujenzi na kupiga marufuku uagizwaji wa vifaa hivyo nje ya nchi.

Waziri Dkt. Jafo ameyasema hayo leo Julai 19,2024 Jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kukagua na kuona maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Shirika la Viwango Tanzania (TBS) huku akisisitiza kuwa ujenzi wowote utakao anza vifaa vinunuliwe ndani ya nchini.

"Vipo viwanda vikubwa ndani ya nchi viwanda hivyo badala ya kuzalisha China wameamua kuja kuzalisha Tanzania na vina masoko Kenya Burundi, Uganda na Kongo sasa ninavyosikia jengo limechelewa kwa kuagiza vioo nchini China nawashangaa, " amesema Dkt. Jafo.

Waziri Jafo ameridhishwa na kazi inayoendelea na matarajio ifikapo Oktoba 15,2024 ujenzi uwe umekamilika.


"Kwa kweli nawapongeza kwa ujenzi huo wa jengo kwani linaendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali ya shilingi bilioni 24",amesema

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Needpeace Wambuya, amesema kwa ujezi wa jengo hilo unakwenda kusogeza huduma ya haraka kwa upimaji ubora wa bidhaa kwa wadau lakini pia wamechukua maelekezo bidhaa zote zinatumika za hapa nchini.

"Tzasisi zilizopo chini ya Wizara ziwe mfano kuhakikisha bidhaa zote zinazotumika kwenye ujenzi zinatoka ndani ya nchi kwa kulinda viwanda vetu, ajira na tupunguze fedha za kigeni, " amesema Bw.Wambuya

Naye Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati, Nickonia Mwambuka ameshukuru kwa ziara hiyo ya Waziri na kuahidi kuwa hadi kufikia Oktoba 15,2024 Jengo hilo litakuwa limekamilika na watafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu ili jengo hilo likamilike kwa wakati.

"Pia watalifanyia kazi suala maabara kwani ujenzi huo wa maabala utasaidia mikoa ya Kanda ya kati wajasiriamli na wafanyabishara itakuwa rahisi kuchukua sampuli kupimwa na kupata majibu kwa wakati",amesema.

Hata hivyo Ujezi wa jengo hilo la TBS lina thamani ya shilingi bilioni 24.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo,akizungumza na wadhibiti ubora wakati alipotembelea Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) leo Julai 19,2024 jijini Dodoma.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo,akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo,akitoa maelezo wakati akikagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo,akizungumza mara baada ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.



WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo,akizungumza mara baada ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Bw.Needpeace Wambuya,akizungumza mara baada ya Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo (hayupo pichani) mara baada ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.




Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya kati, Nickonia Mwambuka,akimpongeza Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt, Selemani Jafo (hayupo pichani) mara baada ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.


Muonekano wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lililopo eneo la Njedengwa, jijini Dodoma,leo Julai 19,2024.
Share:

BONANZA LA MICHEZO NA MAZOEZI KUFANYIKA PEMBA JULAI 20 - 28, 2024


Katika kuadhimisha miaka 10 ya klabu ya mazoezi ya Gombani (Gombani Fitness club), klabu hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) na Shirika ka Bima la Zanzibar wameandaa bonanza la mchezo wa mazoezi lenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika mazoezi na michezo.

Bonanza hilo litakaloshirikisha michezo ya aina mbali mbali litafanyika kisiwani Pemba kuanzia tarehe 20 hadi 28, Julai mwaka huu. Viongozi mbali mbali wa serikali na taasisi binafsi wanatarajiwa kushiriki siku ya Jumapili ya tarehe 28 ambayo ndio itakua kilele cha maadhimisho hayo kwa kuanza na matembezi kutoka Madungu na kumalizikia katika Uwanja wa Mpira wa Gombani, kuanzia saa 12:00 asubuhi.

Jumla ya michezo mitatu itachezwa siku hiyo ikiwemo mazoezi ya viungo, mchezo wa magunia na mchezo wa kuvuta kamba ambayo jinsia zote zitashiriki kwa kuonesha vipaji na uwezo wao.

Katika shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho hayo waandaaji wa bonanza hilo watapita skuli na shehia mbali mbali kuhamasisha kuhusu usawa wa kijinsia katika mazoezi na michezo, pamoja na kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kujikinga na ukatili wa


kijinsia (GBV) kupitia michezo maalum inayojulikana kama (S4D acitivities).

Aidha jumla ya washiriki 500 kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja, Pemba na Tanga wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambapo kauli mbiu ni "Wekeza katika mazoezi na michezo kwa jinsia zote". Kauli mbiu hii inabeba lengo la bonanza hili kwa kuhakikisha watu wote wanahamasika kushiriki katika michezo bila kujali jinsia zao.

Kwa kushirikiana na Shirika la Bima la Zanzibar tunahamasisha Wanamichezo kujikatia bima ya 'Group Personal Accident' (Bima ya ajali kwa Wanakikundi) ambayo itakuwa inawakinga dhidi ya maumivu ya mwili na/au vifo vitakavyosababishwa na ajali wakati wakiwa katika mazoezi na harakati zao za michezo za kila siku.

Wakati Gombani Fitness Club inatimiza miaka 10 tokea kuanzishwa kwake, mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa afya za wana klabu, bado kuna changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwepo kwa miundombinu rafiki ya kufanyia mazoezi kisiwani Pemba hususani kwa wanawake, dhana potofu dhidi ya mazoezi ya viungo, na kukosekana kwa taarifa sahihi juu ya umuhimu wa mazoezi na michezo katika vyombo vya habari.

Kwa sasa TAMWA ZNZ inatekeleza programu ya michezo kwa maendeleo yenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia katika michezo ambayo inatekelezwa kwa pamoja na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD) kwa ushirikiano mkubwa na Taasisi ya Maendeleo ya kimataifa ya Ujerumani (GIZ).

Imetolewa na;

Kamati ya maandalizi,

Bonanza la Michezo na Mazoezi Pemba.
Share:

MFUKO WA HIFADHI YA JAMII WA PSPF KUTOKA ESWATINI WAFURAHIA MAFANIKIO NSSF

Na MWANDISHI WETU

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameushukuru Ufalme wa Eswatini kuja Tanzania kujifunza mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao umekuwa na ustahimilivu wa muda mrefu na unaweza kulipa mafao kwa wanachama wake.

Mhe. Katambi amesema hayo mwishoni mwa wiki katika ofisi za NSSF, Dar es Salaam, wakati akizungumza na ujumbe kutoka Ufalme wa Eswatini ukiongozwa na Mhe. Mabulala Maseko, Waziri wa Utumishi wa Umma, Wabunge na wataalumu kutoka Mfuko wa PSPF chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Sammy Dlamini.

Ujumbe huo ulifika nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu wa mambo mbalimbali yanayofanywa na NSSF kuanzia mabadiliko ukiwa Mfuko wa akiba NPF mpaka kuwa Mfuko wa NSSF, uwekezaji, ukusanyaji michango na kusajili wanachama.

Mhe. Katambi amesema baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, NSSF imefanikiwa kuendesha shughuli zake kidijitali ambapo sasa wanachama wanaweza kupata taarifa zao mbalimbali kupitia simu ya kiganjani bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF jambo ambalo linawaondoshea usumbufu.

Amesema NSSF pia imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo kuwa na ustahimilivu wa muda mrefu na kulipa mafao bila ya kutetereka, umeweka miradi ambayo inatoa huduma kwa wananchi na imekuwa ikizalisha kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanachama na namna inavyolipa mafao kwa wanachama wake kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhe. Maseko amesema wamefurahishwa na hatua mbalimbali ambazo NSSF imepitia tangu kuanzishwa kwake na jinsi inavyofanya vizuri kwenye mifumo na uwekezaji wake.

“Tuko hapa kujifunza kutoka kwa marafiki zetu na kuona jinsi wanavyoendesha Mfuko wao ambao bado ni endelevu kwa kutoa huduma kwa wanachama na kukusanya mapato yake kwa kutumia mifumo mbalimbali,” amesema Mhe. Maseko.

Amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa na manufaa makubwa kwa kupunguza umasikini kwa wananchi, kuleta ustawi wa nchi na ukuaji wa uchumi ambapo inawaweka wananchi katika hali ya usalama kwa kuwa wana uhakika wa kufanya shughuli za maendeleo.

“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa na ustawi mzuri kwa Tanzania, lakini siyo Tanzania tu, tutafurahi kuona mafanikio haya yakinufaisha Afrika kwa ujumla ili kupunguza umasikini,” amesema Mhe. Maseko.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema ujumbe huo wa Eswatini umefika nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu kwa mambo mbalimbali kuanzia uandikashaji wa wanachama, ukusanyaji michango, uwekezaji na kulipa mafao pamoja ilivyoweza kutoka kwenye mfumo wa zamani ambao walikuwa wanalipa mafao ya muda mfupi mpaka kutoa mafao ya muda mrefu.

“Sasa hawa wenzetu walitaka kufahamu tulifanya vipi, tulianza kuchukua hatua gani na tulitumia wataalamu gani mpaka tunafika hapa tulipofikia na wamefurahi sana kwa sababu ni kitu ambacho wanaenda kukifanya katika nchi yao,” amesema Bw. Mshomba.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi wa Mfuko wa PSPF wa Eswatini, Bw. Sammy Dlamini, amesema wamejifunza mambo mengi mazuri yaliyofanywa na NSSF tokea ilipoanzishwa mpaka ilipofikia sasa.

Ujumbe huo wa Ufalme wa Eswatini ulikuwa na watu tisa ukiongozwa na Mhe. Mabulala Maseko, Waziri wa Utumishi wa Umma, Wabunge na wataalam kutoka Mfuko wa PSPF chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Sammy Dlamini.
Share:

MWENYEKITI RAJAB AWAGHARAMIA MADEREVA 600 MAFUNZO

Na Hadija Bagasha Tanga, 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM  Mkoa wa  Tanga Rajabu Abrahaman Abdalah amekabidhi kiasi cha shilingi Milion 30 kama ada kwa ajili ya kuwawezesha madereva wa Daladala na Coaster zinazofanya safari zake ndani ya jiji la Tanga kupata mafunzo katika fani hiyo kwenye chuo cha mafunzo ya ufundi stadi 'VETA' ili kukidhi vigezo vinavyotakiwa kutumia vyombo vya usafiri.

Madereva hao wapatao 600 watapata mafunzo kwa  mwezi mmoja  ndani ya chuo hicho cha ufundi stadi 'VETA' Tanga  kikishirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani  lengo likiwa ni kuwaongezea elimu na kuwawezesha kupata leseni ili kukidhi vigezo vya sheria za usalama barabarani ambapo wengine wao wamekuwa wakikamatwa na makosa mbalimbali yakiwemo ya ukosefu wa leseni za udereva.

Akikabidhi fedha hizo katika ofisi ya Chama cha Mapinduzi,  Mwenyekiti Rajabu amewaasa madereva kuendelea  kuzingatia sheria za usalama barabarani huku akiwasisitiza kutojihusisha na vitendo vya rushwa pale wanapokamatwa mara baada ya kubainika kufanya makosa mbalimbali. 

"Tukumbuke kuwa tukiendesha vyombo vya moto kiholela  mnachangia kwa kiasi kikibwa sana kuhatarisha maisha yenu wenyewe madereva  lakini pia na wale ambao mnawaendesha kwenye vyombo vya moto  , ni wajibu  wa Serikali kuhakikisha inasimamia miongozo na sheria tuliyojiwekea kwa maslahi ya watanzania." amesema Abdulrahmani.

"Ni vibaya sana kumuona askari barabarani amekukamata na akakutoza faini kwa sababu ya uzembe wako mwenyewe halafu unakwenda kumuona ni mbaya lazima tupeane elimu na kuambiana sisi wenyewe kwa wenyewe, usifanye mapatano na askari pale unapokamatwa ukimkuta askari ambaye sio muadilifu, mpenda rushwa  sasa ili yasitokee haya lazima tufuate utaratibu tutumie vyombo vya moto vikiwa vimetimia na kukidhi vigezo" alisisitiza.

Rajabu ambaye ni mjumbe wa halmashauri kuu Taifa  na mjumbe wa kamati ya CCM Taifa  ameongeza kwa kusema kuwa viongozi  wa Serikali kwa kushirikiana na Chama ngazi ya  mkoa huo  watahakikisha  wanaendelea kuwainua wananchi wanaojishughulisha na shighuli za kujipatia kipato wakiwemo wajasiriamali wadogo wadogo ili  kuwainua kiuchumi kwa hali na mali.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya kamanda wa kikosi cha usalama barabarani " RTO" Mkoa wa Tanga Inspekta Rajabu Ngumbi amekiri kuwepo  kwa wimbi la madereva wengine ambao wamekuwa wakikamatwa kwa makosa mbalimbali ya kutokuwepo na leseni kama sheria za usalama barabarani zinavyotaka ambapo amesema kwa msaada huo walioupata madereva wengi wataweza kupata uhalali wa kuendelea na kazi zao.

Inspector Ngumbi amewaasa madereva kuchangamkia fursa hiyo ambayo itawasaidia kupata ajira kupitia makampuni na viwanda mbalimbali vilivyopo hapa nchini hususani katika jiji la Tanga. 

"Hiki kilikiwa ni kilio chenu madereva cha muda mrefu sana viongozi wameshafanya yao sasa palipobakia ni nyie kutekeleza  niwaombe sana  msituangushe  tumebahatika kuwa na viwanda vingi lakini tusijekuwa watazamaji  mwekezaji anapokuja kuwekeza anategemea asilimia tisini ya madereva watoke  ndani ya jiji la Tanga"
Amesema Inspector Ngumbi.

Kwa upande wao mwenyekiti  wa muungano wa wasafirishaji Abiria ndani ya jiji la Tanga 'MUWATA'  Salim Jumbe pamoja na mwenyekiti wa chama cha 'TAREMIA' Ismail Masoud wamemshukuru na kumpongeza mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga kwa hatua hiyo aliyoifanya kuwashika mkono madereva ambao wengi wamekuwa wakishindwa kufanya shighuli hiyo kwa kukosa vigezo ikiwemo leseni za udereva.

Mkuu wa chuo cha ufundi stadi 'VETA' jiji la Tanga  Gideoni Olelairumbe amesema kuwa kwa kuzingatia sheria na miongozo vya nchi juu ya ufundi stadi watahakikisha kwa kushirikiana na ofisi ya kamanda wa Polisi kikosi cha usalama barabarani pamoja na Mamlaka ya mapato Tanzania 'TRA' madereva wote wanamaliza masomo yao kwa viwango vinavyotakiwa.

"Hawa madereva tutakuwa nao pale VETA' kwa muda wa mwezi mmoja tutawagawa kwenye mkundi kulingana na mahitaji yao kwa sababu tunaamini wana mahitaji ya aina mbalimbali na ndio lengo letu la VETA hivyo nimewapokea vijana hawa tutatekeleza kama kanuni za nchi zinavyotaka kwa kushirikiana na ofisi ya TRO na TRA.

Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger