Tuesday 20 April 2021

Dkt. Kalemani : Marufuku kuuza mafuta yasiyo na vinasaba

...


 Na Zuena Msuya Dodoma,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amepiga marufu uuzaji wa mafuta ya Petroli, Dieseli, na Mafuta ya Taa yasiyo na vinasaba unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara nchini.

Dkt. Kalemani alitoa maagizo hayo Jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kushtukiza ya kukagua vinasaba kwenye mafuta yaliyopo katika vituo vya kuuzia mafuta mkoani humo, iliyofanyika Aprili 20, 2021.

Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali na Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi wa wizara hiyo, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini( EWURA),Mhandisi Godfrey Chibulunje.

Dkt. Kalemani Alisema kuwa vinasaba vinadhihirisha viwango na ubora wa mafuta nchini.

“Maelekezo yangu kwa wauzaji wa mafua nchini ni lazima muendelee kuuza mafuta yenye vinasaba kwa sasa ili kujiridhisha na kiwango na ubora wa mafuta nchini, na kama mafuta hayana vinasaba ni marufuku kuyachukuwa na kuuza, kuna minong’ono katika baadhi ya maeneo kuwa kuna mafuta yanayouzwa ya aina hiyo, tutakayembaini tutachukua hatua stahiki”, alisema Dkt. Kalemani.

Katika ziara hiyo, hakuna kituo hata kimoja kilichobaininika kuuza mafuta yasiyo na vinasaba.

Alieleza kuwa kwa sasa Shirika la Viwango nchini (TBS), ndiyo llililopewa kazi ya kupima na kuweka vinasaba katika mafuta yote yanayoingia nchini ili kudhibiti ubora na tayari kazi hiyo imeanza kufanyika.

Alisisitiza kuwa kuanzia sasa mafuta yote nchini yatakuwa yakipimwa na kuwekwa vinasaba na TBS na ikibainika kuna mafuta ambayo hana vinasaba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watendaji husika.

“TBS ni chombo cha serikali, kinachofanya kazi ya kudhibiti ubora na viwango ikiwepo wa mafuta nchini hivyo kuanzia sasa ndiyo kifanya kazi ya kupima na kuweka vinasaba kwenye mafuta yote nchini, endapo atatokea mwingine mtaelekezwa na serikali”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Lengo la serikali kuipa TBS kazi ya kuweka vinasaba katika mafuta yote nchini ili kuokoa fedha za serikali zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa mwezi ambazo awali alikuwa akilipwa aliyekuwa akifanya kazi hiyo.

Vilevile ni kuijengea uwezo taasisi hiyo na kuongeza ajira kwa watanzania.

Katika ziara hiyo, aliitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji kuwachukulia hatua waafisa wawili katika idara ya manunuzi wa Mamlaka wa Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini( EWURA), pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi wa taasisi hiyo kwa kushindwa kutekeleza maelekezo ya serikali kwa wakati.

Dkt. Kalemani alisema kuwa watumishi hao, hawakutekeleza maagizo ya serikali yaliyotolewa tangu Februari 5, 2021, kwa sababu zao wenyewe, pia wachunguzwe kwa nini hawakutekeleza maagizo hayo, na kusababisha migogoro.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger