Friday 3 December 2021

MTOTO ACHOMWA KWA MKASI WA MOTO AKITUHUMIWA KUIBA 'FLASH' YA MOVIE SHINYANGA MJINI


Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo  kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo.
Muonekano wa sehemu alizojeruhiwa mtoto huyo  kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9 anayesoma darasa la tatu shule ya Msingi Bugoyi A Mjini Shinyanga amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kuunguzwa na mkasi wa kukatia fensi uliochemshwa kwenye jiko la mkaa akituhumiwa kuiba ‘Flash’ ya mama na bibi yake.


Mashuhuda wa tukio wameiambia Malunde 1 blog kuwa mtoto huyo alifanyiwa ukatili huo Desemba 1,2021 majira ya saa 2 usiku katika mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.

Wameeleza kuwa siku ya tukio jioni alipewa Flash na bibi yake aitwaye Adelida Leonard (50) na mama yake mzazi Beatrice Mwombeki (28) ili aende eneo jirani akaweke Movie (Filamu) kwenye ‘Flash’ lakini akiwa njiani alidondosha Flash hiyo na kurudi nyumbani kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Flash hiyo.

“Baada ya mtoto huyo kurejea nyumbani na kuwaelezea bibi na mama yake kuwa Flash imepotea,walimwambia aende akaitafute lakini hakufanikiwa kuipata na akaogopa kurudi nyumbani na ilipofika usiku alirejea nyumbani ndipo akafanyiwa ukatili kwa kuchomwa na kipande cha mkasi wa kukatia maua/ fensi kilichochemshwa kwenye jiko la mkaa sehemu mbalimbali za mwili wake hasa mgongoni na mapajani na kumsababishia majeraha”, wamesema mashuhuda wakizungumza na Malunde 1 blog.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema chanzo cha tukio ni kumtuhumu mtoto huyo kuwa ameiba Flash na kwamba mbinu iliyotumika ni kuchemsha kipande cha mkasi wa kukatia fensi kwenye jiko la mkaa kisha kumuunguza sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema watuhumiwa ambao ni Adelida Leonard (bibi) na Beatrice Mwombeki (mama mzazi) wamekamatwa na madhura amelazwa katika hospital ya rufaa mkoa wa Shinyanga.

Share:

BENKI YA CRDB YAAHIDI MITAJI NA MIKOPO KWA WAFANYABIASHARA, WAWEKEZAJI KUTOKA ITALIA


Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake kwa wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Sehemu ya Wafanyabiashara na Wawekezaji walishiriki katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Sekta ya Hoteli Zanzibar, Paulo Rosso walipokutana katika Jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Benki ya CRDB imewahakikishia wafanyabiashara na wewekezaji wa Tanzania na Italia utayari wake wa kutoa mikopo na mitaji ya kutosha watakapo kuwa tayari kuwekeza nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Itali liloandaliwa na ubalozi wa Tanzania lililofanyika Jijini Roma, nchini Italia.

Nsekela amesema Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoendana na huduma za kibenki zinatatuliwa.

“Nawahakikishia kuwa Benki ya CRDB itawawezesha mikopo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu mitaji ya kuwekeza ipo karibuni sana tuijenge Tanzania,” amesema Nsekela.

Nsekela ameongezea kuwa Benki ya CRDB inafarijika kuona wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza zaidi Tanzania, huku akimpongeza Balozi wa Tanzania nchini Itali, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo kwa kuandaa Jukwaa hilo ambalo limetoa fursa ya kueleza sekta mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.

“Benki ya CRDB pamoja na mambo mengine tutahakikisha kuwa sisi kama benki tunawawezesha wawekezaji wanaowekeza nchini na kuwapa mitaji ya biashara pamoja na biashara za kimataifa kati ya nchi moja na nyingine…,” alisisitiza.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo ameipongeza Benki ya CRDB kwa utayari wake wa kusaidiana Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia utoaji wa mikopo na mitaji, pamoja na huduma nyengine za kifedha zinazoongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashira.

“Benki ya CRDB imeonyesha uzalendo mkubwa kwa kushirikiana na Serikali kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini, binafsi sina shaka na uwezo wao kimtaji. Nimefurahi pia wamekwenda mbele zaidi kwa kutoa huduma za ushauri katika uwekezaji, hii inaonyesha ni jinsi gani wamejipanga vizuri,” amesema Balozi Kombo.

Naye, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.

“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza….nawahakikishia mimi nimewekeza Tanzania na ninaona ni sehemu salama ya kuwekeza karibuni sana kuwekeza kwa maendeleo ya Tanzania na Italia,” amesema Bw. Rosso

Jukwa hilo la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji takribani 250 kutoka nchi zote mbili. Wafanyabiashara na wawekezaji hao ni wa sekta za utalii, kilimo, madini, na ujenzi.

Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
--
Share:

WANANCHI WAFANIKIWA KUMUUA FISI ALIYEUA MBUZI 6 MJINI KAHAMA

Wananchi wa kijiji cha Bujika Kata ya Nyandekwa katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamefanikiwa kumuua mnyama aina ya Fisi aliyewaua mbuzi sita usiku wa kuamkia leo Disemba 03, 2021.

Fisi huyo alivamia banda la Mbuzi wa Mzee Keneth Shaban majira ya saa tano usiku na kuwashambulia Mbuzi waliokuwa ndani ya banda hilo ambapo imeelezwa kuwa baada ya fisi huyo kuingia katika banda hilo mlango ulijifunga na kushindwa kutoka.

Akizungumzia tukio hilo Afisa Maliasili msaidizi wa Manispaa ya Kahama, Thomas Manumbu amesema baada ya kupata taarifa hizo walifika eneo la tukio na walikuta tayari wananchi wamemuua fisi huyo ambapo mbali na kuua Mbuzi hao hakuna mtu aliyethurika.

"Tulipata taarifa kutoka kwa katibu tawala kuhusiana na tukio hilo ni kweli limetokea lakini halidhuru mtu yoyote kikubwa tu limesababisha Mbuzi hao kuuliwa na mnyama huyo",amesema.

Hata hivyo  amewataka viongozi wa serikali za vijiji na kata kuimarisha kamati za ulinzi na usalama katika maeneo yao ili kukabiliana na wanyama hao ambao wamekuwa wakisababisha madhara kwa binadamu pamoja na mifugo.

CHANZO- HUHESO FM
Share:

SATURA ATOA UFAFANUZI TOZO ZA TAKA ZILIZOZUA MJADALA SHINYANGA MJINI "SIYO TOZO MPYA, NI JUKUMU LA JAMII KUZOA TAKA"

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021 
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Jomaary Satura ametoa ufafanuzi kuhusu mjadala unaoendelea kuhusu ada za uzoaji wa taka ngumu akisema tozo hizo ambazo zinalalamikiwa na wananchi kuwa ziko juu kuwa siyo tozo mpya bali zipo kwa mujibu wa sheria ndogo ya Manispaa ya Shinyanga iliyopitishwa mwaka 2014 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019.


Akizungumza na Waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 3,2021, Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Shinyanga amesema ada hizo za uzoaji taka zilizoanza kutozwa kwa wananchi Desemba 1,2021 kupitia kwa kampuni ya Ukandarasi ya Networking Youth Group ya Jijini Arusha siyo tozo mpya.

“Kumekuwa na mijadala kuhusu tozo za uzoaji taka ngumu katika Manispaa ya Shinyanga. Napenda kuwaeleza wananchi kuwa hizi tozo zinazotozwa sasa hivi siyo tozo mpya bali zinatokana na Sheria ndogo ya Manispaa ya Shinyanga ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ambayo ilizingatia hatua zote muhimu ikiwemo kujadiliwa na wananchi, Baraza la Madiwani na kupitishwa na Waziri mwenye dhamana”,amesema Satura.

“Kwanini mabadiliko haya yanaonekana sasa badala ya kutumika tangu sheria ilipotungwa?,Kwanza naomba niweke wazi kuwa jukumu la kuzoa taka ngumu ni wajibu wa mwananchi na wajibu wa kuteketeza taka ni jukumu la Serikali. Siku za nyuma Halmashauri haikumtwisha mwananchi mzigo wa kuzoa taka hivyo shughuli za uzoaji taka na kuzipeleka kwenye dampo zilikuwa zinafanywa na Halmashauri kupitia vikundi vya kijamii. Halmashauri ilikuwa inatumia takribani shilingi Milioni 30 kila mwezi kwa ajili ya uzoaji taka, jukumu ambalo siyo lake, hivyo tulikuwa tunaisaidia jamii”,amesema Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga.

“Siyo wajibu wa Halmashauri ya Manispaa kuchukua taka kutoka kwenye maghuba na kupeleka kwenye dampo.Tulikuwa tunabeba jukumu hilo,tumeona hizo gharama ni bora zirudi kwa wananchi wenyewe. Sisi tumejiondoa kwenye uzoaji taka kutoka kwenye maghuba kwenda kwenye dampo. Wajibu wa jamii ni kukusanya taka na kuzipeleka kwenye dampo na sisi wajibu wetu kama Serikali ni kuteketeza taka ngumu kwa kuzingatia aina za taka”,amefafanua Satura.

Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imekabidhi Sheria ndogo iliyopitishwa mwaka 2014 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa Kampuni ya Networking Youth Group ya Jijini Arusha ambayo inakusanya taka kwa kutumia magari katika kata tano za kimkakati ambazo ni Kambarage, Mjini, Ngokolo, Ibinzamata na Ndembezi na kwenye kata zingine vikundi vya kijamii vitaendelea kukusanya taka ngumu.

“Huyu Mkandarasi anayekusanya taka tumempatia sheria hizi na hizi tozo siyo mpya. Sheria inasema hivyo hakuna aliyezipanga hivyo wananchi waendelee kulipia tozo hizi ili kuhakikisha tunaondoa taka katika Manispaa yetu ambayo tunataka iwe Jiji”,amesema.


Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo kuwataka Viongozi wa serikali za mitaa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ada za uzoaji taka ngumu kwenye maeneo yao ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Zoezi la uzoaji wa taka ngumu likiendelea katika ghuba la Soko Kuu Mjini Shinyanga
Ufafanuzi huo wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga unatokana na malalamiko ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga  ambao wanasema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imepandisha ghafla ada za uzoaji wa taka ngumu kuanzia Desemba 1,2021 kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga .

Katika malalamiko hayo mfano wamesema mtu aliyekuwa analipa shilingi 2,000/= sasa atalipia shilingi 5000/= na upande wa taasisi zilizokuwa zinalipa shilingi 3000/= sasa watalipa shilingi 10,000/= huku aliyekuwa analipia shilingi 10,000/= sasa atatakiwa kulipa shilingi 50,000/= kwa mwezi.

Kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wanasema licha ya kwamba jambo la ada za taka ni la lazima lakini ada hizo mpya ni kubwa kuliko gharama za awali hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza ada hizo.

Share:

WAHUNI 12 WANAOKWAPUA SIMU KWA BODABODA WAKAMATWA



Jeshi la Polisi katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya, imefanikiwa kukamata simu zaidi ya 30 na watuhumiwa 12 wa matukio ya uporaji wa simu, wengi wakiwa ni wale wanaotumia bodaboda na visu kufanya uhalifu huo.

Watuhumiwa hao wamekamatwa katika oparesheni maalum iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini Kenya katika maeneo ya Githogoro, Murera na Kiambu ambapo watuhumiwa hao, hujifanya ni madereva bodaboda kabla ya kuwapora abiria na watembea kwa miguu simu zao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kiambu, Mohamed Badel amesema watuhumiwa hao, hufurika katika mitaa ya Mji wa Kiambu kuanzia majira ya saa kumi alfajiri hadi saa kumi na moja, muda ambao watu wengi hutoka majumbani mwao kuelekea makazini.

Badel amesema waliamua kuendesha oparesheni maalum baada ya kusikia malalamiko ya mara kwa mara ya wakazi wa mji huo ambapo kwa kushirikiana na wasamaria wema, walifanikiwa kuwanasa wahalifu hao.

Ameongeza kuwa watuhumiwa wote wapo rumande na wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Kiambu kusomewa mashtaka yanayowakabili na kuwataka madereva wa bodaboda wanaozingatia sheria, kujiandikisha na kupewa namba maalum zitakazowatofautisha na wahalifu.

Pia amewataka watu walioibiwa simu zao, kufika katika Kituo cha Polisi cha Kiambu ili kuzitambua simu zao.
Share:

JAMBAZI AJISALIMISHA POLISI...AAHIDI KUWA RAIA MWEMA




Mwanaume mmoja, Faida Komanya (34) mkazi wa Kijiji cha Bugalagala Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ambaye alikuwa akituhumiwa na Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na vitendo vya ujambazi, amejisalimisha kwa jeshi hilo na kuomba apelekewe kama raia mwema baada ya kujirekebisha tabia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe, amesema mwanaume huyo amehusika katika matukio mengi ya kijambazi na aliwahi kufungwa katika Gereza la Butimba, Mwanza.

Kamanda Mwaibambe ameongeza kuwa kwa mujibu wa Komanya, ameamua kujisalimisha baada ya kupoteza ndugu wengi kwa kuuawa pamoja na kutengwa na ndugu wengine pamoja na jamii.
Share:

NSSF YATUNUKIWA TUZO KUTHAMINI MCHANGO WAKE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI


Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Ekwabi Mujungu (kushoto), ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, akipokea tuzo na cheti kutoka kwa Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, kwa ajili ya kuthamini mchango wa NSSF katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Ruanda Nzovwe mkoani Mbeya. Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko.
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala (NSSF), Ekwabi Mujungu (wa tatu kulia) ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa NSSF baada ya kupokea tuzo na cheti kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuthamini mchango katika katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Wa tatu kushoto ni Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Deus Jandwa.
Tuzo na cheti kutoka TACAIDS cha kuthamini mchango wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika mapambano dhidi ya UKIMWI
HUDUMA: Wananchi walipokuwa wanahudumiwa kwenye banda la NSSF wakati wa maonesho ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yenye kauli mbiu 'Zingatia usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko ' , yanayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya, ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unashiriki kutekeleza Sera ya Utumishi wa Umma kuhamasisha elimu juu ya VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi
Katibu Mahsusi ambaye pia Mwelimishaji rika wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii(NSSF) Mkoa wa Mbeya, Happy Gwimile (wa kwanza Kulia) akiwakumbusha baadhi ya wananchi waliotembelea banda la NSSF kuhusu kuendelea kujikinga na maambukizi VVU na UKIMWI hasa mahali pa kazi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.
Afisa Mkuu Utawala Daniel Shaidi (kushoto) wa NSSF Makao Makuu ambaye pia ni Mwelimishaji rika mahala pa kazi, alipokuwa anamuelekeza Fatma Fungo (kulia), namna ya kutumia mifumo mbalimbali inayomwezesha mwanachama kuangalia taarifa zake kupitia simu ya kiganjani bila kulazimika kufika katika Ofisi za NSSF. Mifumo hii ni pamoja na NSSF Taarifa , Whatsapp na ujumbe mfupi wa maneno yaani SMS. Mifumo hii ya kidigitali inamrahisishia mwanachama kupata huduma kwa haraka kwa kujihudumia mwenyewe, inampunguzia gharama za usafiri. Maonesho ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duaniani Kitaifa yanafanyika katika Mkoa wa Mbeya.
Katibu Mahsusi ambaye pia Mwelimishaji rika wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii(NSSF), Ng’walu Mihambo kutoka NSSF Tarime, akitoa maelezo kwa wananchi juu ya mbinu za kuzuia magonjwa ya VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na ulaji unaofaa, mazoezi ya mwili, kuwa na uzito usiozidi kiasi kulingana urefu, kuepuka matumizi ya pombe na sigara, VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyo ambukizwa
Afisa Mwandamizi Utawala, Naphisa Jahazi ambaye pia ni Mwelimishaji rika mahala pa kazi kutoka NSSF, Mkoa wa Temeke akielezea kwa baadhi ya wananchi namna NSSF ilivyojielekeza katika kudhibiti VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukizwa mahala pa kazi, wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duaniani Kitaifa yanafanyika katika Mkoa wa Mbeya
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), haujawaacha nyuma makundi yenye mahitaji maalum, Mkalimani wa Lugha ya alama Baraka Bakari (wa kwanza kulia) akiwatafsiria walemavu wa usikivu elimu kuhusu hifadhi ya jamii, walipotembelea banda la NSSF wakati wa Maonesho ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Mbeya
  *****

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepewa tuzo kama ishara ya kuthamini mchango wake katika mapambano ya VVU na UKIMWI.


Tuzo hiyo ilitolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na kukabidhiwa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, wakati wa maadhimisho ya siku ya UKiMWI duniani yaliyofanyika jijini Mbeya.


NSSF imekuwa ikitekeleza Sera ya UKIMWI mahala pa kazi na imekuwa ikisimamia miongozo yote inayohusu VVU na UKIMWI


Pia, Mfuko ulishiriki katika maonesho na maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ili kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa Taifa kuendelea kujikinga na masuala ya VVU na UKIMWI.


Mkurugenzi Mkuu Bw. Masha J. Mshomba katika salamu zake kwa wafanyakazi wa Mfuko katika siku ya UKIMWI duniani alisema “Nasisitiza kuwa, ni wajibu wa kila mfanyakazi kuchukua hatua katika kudhibiti VVU na UKIMWI ili kuokoa nguvu kazi ya Mfuko na Taifa”.


Aidha, Mshomba alifafanua zaidi na kusema kwamba NSSF inayo sera inayohusu masuala ya VVU na UKIMWI ambayo inasisitiza kujilinda, kujikinga, kumlinda mfanyakazi aliyeathirika, kuzuia unyanyapaa na kumsaidia mfanyakazi aliyeathirika.
Kauli Mbiu ya mwaka huu ilikuwa “Zingatia Usawa, Tokomeza Ukimwi, Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko”.

Share:

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO IJUMAA DESEMBA 3,2021

Magazetini leo Ijumaa December 3 2021
















Share:

Thursday 2 December 2021

WAKULIMA ARUSHA WAPEWA ELIMU YA USAJILI WA VYAMA VYA UMWAGILIAJI NA UCHANGIAJI WA ADA NA TOZO


Picha ikionesha wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kikao cha pamoja na Afisa Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Arusha,hayupo pichani wakijadili kwa pamoja maswala ya tozo za Umwagiliaji.
Bi. Fatuma Mwera,Afisa Kilimo toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akiongea na viongozi wa skimu za umwagiliaji katika wilaya ya Arusha kuhusiana na maswala ya Tozo na Ada za umwagiliaji.
Kulia Kaimu Mkurugenzi wa Mipango toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Reginald Diyamet na Mhandisi Naomi Mcharo, wakijadili jambo linalohusu Kilimo cha Umwagiliaji kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020.

***

Na Mwandishi wetu – Arusha

Wakulima katika skimu za kilimo cha umwagiliaji Mkoani Arusha, wamepewa elimu kuhusiana na namna ya kusajili vyama vya umwagiliaji na utoaji wa ada na tozo na kupewa utaratibu wa kulipia ada hizo zitakazosaidia kuboresha na kurekebisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji pale itakapokumbwa na madhara yatokananyo na athari za mabadiliko ya tabianchi au uchakavu.

Bi Fatuma Mwera Afisa Kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akizungumza na baadhi ya viongozi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji katika Halmashauri ya Arusha katika kata ya Ilikiding’a alibainisha kuwa, usajili wa vyama vya umwagiliaji utasaidia skimu kutambulika na kupata fursa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kupelekewa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Aidha aliwaasa viongozi hao kuwa vinara katika suala zima la usimamizi na utunzaji wa mazingira hususan vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kutokufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo.

Aliendelea kusema kuwa, skimu zote za kilimo cha umwagiliaji zitafanyiwa maboresho kwa awamu lakini , skimu ambazo zimesajiliwa ndizo zitakazopewa kipaombele kwanza wakati wa maboresho hayo. “ Ni vizuri kusajili wote kwa pamoja ili tupange mipango ya kazi kirahisi na kuzifikia skimu kwa awamu",alisisitiza.
Share:

ADA MPYA ZA UZOAJI TAKA MJINI SHINYANGA ZAZUA GUMZO... MKURUGENZI WA MANISPAA KUTOA UFAFANUZI KESHO


Zoezi la uzoaji wa taka ngumu likiendelea katika ghuba la Soko Kuu Mjini Shinyanga leo Novemba 2,2021
Nyaraka ya Jedwali la ada za uzoaji wa taka ngumu kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga linalosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wamepatwa na mshangao baada ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupandisha ghafla ada za uzoaji wa taka ngumu kwa mujibu wa sheria ndogo za Manispaa ya Shinyanga hali ambayo imezua mijadala mbalimbali mtaani na kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutumika Desemba 1,2021.

Katika malalamiko hayo mfano wamesema mtu aliyekuwa analipa shilingi 2,000/= sasa atalipia shilingi 5000/= na upande wa taasisi zilizokuwa zinalipa shilingi 3000/= sasa watalipa shilingi 10,000/= huku aliyekuwa analipia shilingi 10,000/= sasa atatakiwa kulipa shilingi 50,000/= kwa mwezi.

Kupitia majukwa mbalimbali ya mitandao ya kijamii wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wanasema licha ya kwamba jambo la ada za taka ni la lazima lakini ada hizi mpya ni kubwa kuliko gharama za awali hivyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza ada hizo huku wakiomba ulipaji wa ada ya taka uendane na thamani ya fedha na kusisitiza wakusanya taka kukusanya taka kwa wakati kwani wamekuwa wakichelewa kuchukua taka.


Wamesema hali ya zoezi la ukusanyaji wa taka katika Manispaa ya Shinyanga limekuwa halina tija kwa kuwa wananchi wenyewe wamekuwa wakitumia vifaa vyao na gharama zao kuondoa taka kutoka kwa watu wengine wa mitaani na kubainisha kuwa wahusika wa Manispaa wa kuondoa taka kutofikia mitaa yao.


“Hii tozo ya taka inatisha mfano Hotel jana tumeambiwa kutoka 10,000/= mpaka 50000. hii ni asilimia ngapi imeongezwa? kweli inashangaza sana , lakini pia hawa wakusanya taka hawakusanyi taka kwa wakati mara nyingi hadi tunatafuta watu binafsi wenye matolori tunalipa wenyewe maana taka zinajaa na hawaijii ,hili ongezeko la tozo za taka linaumiza wananchi”, wamesema wananchi.


“Utaratibu wa kutaka kupandisha hata sent moja kwenye halmashauri zetu nijuavyo hatua zinazotakiwa ni vikao vya wadau husika , vikao vya Madiwani na Waziri husika kisha wanatuletea wananchi, sasa hatuoni hatua ya 1 na 3. Ipo hivi, hata bunge linapitisha sheria na haiwezi kutumika mpaka Mhe. Rais atie mkono kwa kua- ascend”,wamesema.


“Je mnaweza kutuletea pia wapi Waziri mwenye dhamana alikubali sheria hii ndogo itumike!?, Unaweza tuwekea mihtasri ya vikao vya wananzengo kukubali kupanda kwa ada/ ushuru huu!? Kama hakuna hivyo viwili, jamaa watakuwa wamepandisha isivyotakiwa”, wamesema.


Hata hivyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Jomaary Mrisho Satura alipotafutwa kwa njia ya simu na waandishi wa habari amesema kesho Ijumaa Desemba 3,2021 atakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutolea ufafanuzi suala hilo la ada za uzoaji wa taka ngumu .
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger