Monday 30 March 2020

Tahadhari Ya Corona: Ratiba Ya Bunge Litakaloanza Kesho Yabadilika

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma
Vikao vya Bunge  la bajeti  kuu  vinatarajia kuanza kesho huku utaratibu mpya  ukiwekwa juu ya tahadhari ya Corona ambapo wataruhusiwa kuingia wabunge 150 pekee ukumbini tofauti na  ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Machi ,30,2020 jijini Dodoma  Spika Wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Job Ndugai amesema kutokana na tahadhari ya Ugonjwa unaotokana na virusi vya corona[COVID-19] idadi ya wabunge watakaokuwa wakiingia ukumbini ni  wasiopungua 150  kati ya wabunge 393 .

Amesema kwa kawaida vikao vya  Bunge huhudhuriwa na zaidi ya watu 700 ukumbini ikijumuisha na watumishi wengine bungeni hivyo kutokana na tahadhari ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona wabunge wengine watakuwa wanafuatilia kupitia Mitandao na watagawanyika katika kumbi mbalimbali zilizopo bungeni.

Aidha,Mhe.Ndugai amesema masaa ya vikao vya bunge yamepunguzwa  ambapo vikao vyote vya bunge vitakuwa vinafanywa kwa masaa yasiyozidi manne kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi jioni isipokuwa siku ya kesho.

Kuhusu Maswali na Majibu bungeni Mhe.Ndugai amesema wabunge watakuwa wanapata fursa ya kuuliza maswali kupitia Mtandao  wa Bunge hivyo hakutakuwa na Maswali ya ana kwa ana pia Maswali ya papo kwa  hapo kwa Waziri mkuu hayatakuwepo.

Katika kupiga kura za Ndiyo au Hapana kuhusu kupitisha bajeti Mhe.Ndugai amesema kura hizo zitapigiwa kupitia mtandaoni ambapo pia amebainisha kuwa Waziri mwenye dhamana husuka atalazimika kujibu swali akiwa anatumia kipaza sauti [mic] cha kwenye kiti alichokalia na hatolazimika kuchangia kipaza sauti kimoja kwa Mawaziri wengi kama ilivyokuwa awali.

Ikumbukwe kuwa katika bunge hili la Bajeti kuu  Jumla ya Maswali 525   yatakuwepo ambapo mkutano huo unaanza Machi 31 ,2020 hadi Juni 30,2020    Bunge  litakapovunjwa kwa ajili ya Uchaguzi mkuu 2020.


Share:

MEYA TANGA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUTHAMINI IMANI ZA WATU

Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani
MSTAHIKI meya wa Jiji la Tanga Alhaji Mustapha Selebosi akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani leo kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Meja Mstaafu Mkoba
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji akizungumza wakati wa kikao hicho kulia ni Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa na kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji hilo Alhaj Mustapha Selebosi
MKUU wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa kushoto akipimwa joto na Afisa Afya wa Kituo cha Magaoni Farida Mohamed kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa Halamshauri ya Jiji la Tanga kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani
MKUU wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa kulia akipiga dua sambamba na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji kushoto na Mstahiki Meya wa Jiji hilo Alhaj Mustapha Selebosi kwa ajili ya kumuomba Mungu aliepushe Taifa na Ugonjwa wa Corona
Madiwani kutoka maeneo mbalimbali wakifuatilia kikao hicho
Diwani wa Kata ya Msambweni (CUF) Abdurahaman Hassani akichangia kwenye kikao hicho leo


MSTAHIKI meya wa Jiji la Tanga Alhaji Mustapha Selebosi amepongeza Rais Dkt John Magufuli kwa kuthamini imani za watu ambapo kwa waislamu wanaendelea kufanya ibada zao misikitini na wakristo wanaendelea kufanya ibada zao kanisani.

Meya Sellebosi aliyasema hayo leo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani ambapo alisema kwamba Rais Magufuli amekuwa ni kielelezo tosha kwamba ni kiongozi ambaye anathamini imani za wananchi wake na ndio maana ibada zinaendelea kwenye maeneo mbalimbali.

Alisema kwamba lazima wawe makini na ugonjwa huo wa Corona huku akieleza kwamba kwa wale wenye mitandao wanaosoma kila siku wanatambua adhari ambazo zimetokana na ugonjwa huo duniani

Mstahiki Meya huyo alisema wakati wanawasiliana na jamaa zake wanaokaa Italia wanasema hakuna shughuli hata moja inayofanyika nchini humo hakuna kutembea wala kukutana kutokana na kila mtu kulazimika kukaa nyumbani kwake.

Aidha alisema hata Mombasa nchini Kenya kuna muingiliono wa familia hata ibada watu bada watu wanafanya majumbani mwao hivyo hatuna budi kumshukuru Rais Dkt Magufuli kwa kuthamini imani za watanzania.

“Leo nichukue nafasi hii kumpoingeza Rais Dkt Magufuli kwa kuthamini imani za watu waislamu tunaendelea kufanya ibada zetu misikitini wakristo tunaendelea kufanya ibada wetu kanisani “Alisema

Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji alisema kwamba Jiji hilo limejipanga kuhakikisha linakabiliana na ugonjwa wa Corona kwa kuchukua hatua ya kuweka vifaa maalumu vya kunawia mikono kabla ya kuingia kupata huduma kwenye taasisiza umma.

Naye kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa aliwaagiza maafisa tarafa wilayani humo kuhakikisha wanasimamia maeneo yote ya kutolea huduma wahakikisha wanakuwa na eneo la kunawia mikono na dawa kabla ya kupata huduma.

“Nataka kupata taarifa ni wapi ambapo hawajatekeleza jambo ..tunatamani tuone taasisi zote na maeneo ya kutolea huduma yaweze kuwa kichocheo kikubwa kutoa elimu kwa kupambana na ugonjwa wa Corona”Alisema
Share:

Wagonjwa Wa Corona Nchini Kenya Wafika 50

Waziri wa Afya wa Serikali ya Kenya Mutahi Kagwe leo Jumatatu Machi 30 ametangaza wagonjwa nane zaidi wa ugonjwa wa virusi vya corona COVID-19 na kufanya idadi ya wagonjwa nchini humo kufikia 50.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation, waziri Kagwe amesema kuwa wagonjwa hao nane wameambukizwa virusi vya corona ndani ya nchi na kutoa tahadhari ya ugonjwa huo kuenea ndani kwa kuwa hakuna maambukizi mapya kutoka nje.

Mpaka Jumamosi Kenya ilikuwa na wagonjwa 38. Jana Jumapili waziri Kagwe alitangaza wagonjwa wapya wanne na kufanya idadi kufikia 42, hivyo idadi ya wagonjwa wapya 12 nchini humo imetangazwa ndani ya siku mbili tu.

Mtu mmoja tayari amepoteza maisha nchini humo kutokana na virusi hivyo.


Share:

Waziri wa Viwanda na Biashara ampongeza mjasiriamali mtanzania aliyebuni kifaa maalumu cha kunawia mikono ili kujikinga na virusi vya Corona.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) leo tarehe 30 Machi, 2020 amepokea kifaa maalumu cha kunawia mikono kilichotengenezwa na mjasiriamali wa kitanzania ndugu. Jonas Urio (Ambaye anatokea katika mkoa wa Manyara).

Mhe. Bashungwa amempongeza sana ndugu Jonas Urio kwa ubunifu wake huu wa kutengeza kifaa kizuri na bora cha kunawia mikono ambacho kinaweza kutumiwa na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi kuhudumia watu mbalimbali kusafisha mikono yao ili kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Mjasiriamali ndugu Jonas Urio ambaye ni mbunifu wa teknolojia hii ameishukuru Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kumpa ushirikiano tangu awali alipoanza ubunifu wake hadi kufikia hatua hii ambapo ameshasajiliwa na ubunifu wake utambulika.

Ndugu Jonas amesema, “Napokea ushauri wa maboresho ya klifaa hiki niliyopewa na Mhe Waziri na Naibu waziri ambao wote kwa pamoja wamefurahia sana ubunifu wangu, naahidi kufanyia kazi maboresho yote haraka ili kifaa hiki kingie sokoni ili kusaidia wananchi kujisafisha mikono na kupambana na ugonjwa huu wa Corona”


Share:

Wizara Nne Zaunda Kamati Mzee Kisangani kuwa Bilionea

Issa Mtuwa – Dodoma
Timu ya wataalam 9 kutoka wizara ya Madini, Wiziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, wizara ya Viwanda na Biashara na Wiziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) imeundwa ili kumsaidia Mjasiliamali wa miaka 60 kutoka mkoani Njombe wilaya ya Ludewa, Reuben Mtitu maarufu Mzee Kisangani ili kutimiza ndoto yake ya kuwa bilionea baada ya kubuni kiwanda kinachotengeneza zana zinazotokana na madini ya chuma.

Kamati hiyo imeundwa leo tarehe Machi 30, 2020 na Mawaziri Wanne wa wizara ya Madini Doto Biteko, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu, OR-TAMISEMI Mwita Waitara na Naibu waziri ya Viwanda na Biashara Mhandisi, Stella Manyanya, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wizara ya madini jijini Dodoma.

Wengine waliohudhuria ni kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Mazingira (NEMC) na Wataalam kutoka wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Akifungua kikao hicho, Waziri Biteko amewaeleza wajumbe hao, kuwa lengo ni kujadili namna ya kumsaidia Mzee Kisangani kwenye kila hatua kutoka mahali alipo ili ikibidi awe bilionea.

Ameongeza kuwa, mzee Kisangani hajui kusoma wala kuandika lakini ameonyesha kitu ambacho kama Serikali inahitaji kumsaidia kwa kila hatua anayohitaji.

Biteko amesema, alipokuwa ziarani mkoani njombe kuanzia Machi 13-16, alitembelea kiwanda chake ambapo kwa namna kilivyo, lakini kinatengeneza zana mbalimbali za chuma kama vile, Mapanga, Fyekeo, Visu, Majembe huku akiwa amewaajiri watu 30, kutokana na uthubutu na juhudi alizonazo.

Waziri Biteko akiwa ziarani katika eneo hilo aliahidi kukutana atakutana na Mawaziri wote wanao husiana na shughuli zake ili kujadili namna ya kumsaidia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mussa Zungu, akichangia namna ya kumsaidia, amesema wizara yake kupitia (NEMC) itahitaji andiko (Bussines Plan) na kwamba wataalam wa eneo hilo watasimama ipasavyo kusaidia Mzee Kisangani kufikia ndoto yake.

Wakati Zungu akihitaji andiko, Biteko amesema tayari Chuo Kikuu cha Mzumbe walishajitolea kumuandikia andiko la biashara (Business Plan) ya kiwanda chake. Naye Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI Mwita Waitara, amesema kila mkoa ulipewa agizo la kuandaa maeneo ya uwekezaji hivyo Mkuu wa Mkoa mkoani humo atatoa eneo maalum kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha Kisangani kwenye eneo lililotengwa.

Kwa upande wake, Naibu wa Viwanda na Biashara Mhandisi, Stella Manyanya amesema kumekuwa na changamoto nyingi za kuwasaidia watu wenye ubunifu hususani kutokana na vipengele vilivyowekwa kisheria suala ambalo huwakatisha tamaa.

Amesema wizara yake kupitia NDC, SIDO na TIRDO kila taasisi itatoa mtaalam kwa ajili ya kumsaidia mjasiliamali huyu ili afikie malengo.

Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Prof. Damian Gabagambi amesema mara baada ya kusoma taarifa za ziara ya waziri wa Madini kupitia vyombo vya habari alituma wataalam kwenda kiwandani hapo na kuona namna gani ya kumsaidia ili kuzalisha chuma na kuongeza uwezo wa uzalishaji.

Waziri Biteko ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho, amesema kwakuwa tunataka kuona matokeo ya huyu Mzee kutokana na nguvu za serikali ndipo iliamriwa kuundwa kwa kamati ya wataalam wa aina mbalimbali ambao ni wizara/taasisi kwenye mabano, Wilfred Machumu (Tume ya Madini), Issa Mtuwa (Wizara ya Madini), Abbas Mruma (GST), Prof. Silvester Mpanduji (SIDO), Prof. Madundo Mtambo Mkumbukwa (TIRDO), Dr. Yohana Mtoni (NDC), Anorld Mapinduzi (NEMC), Leo Mavuka (TAMISEMI), na Dr. Hellen (Chuo Kikuu Mzumbe.


Share:

TAKUKURU Yakanusha Kusambaratisha Mkutano wa Katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa. Kitila Mkumbo

TAASISI ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekanusha taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na Mamlaka hiyo kusambaratisha mkutano wa Katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa. Kitila Mkumbo na wajumbe wa mkutano mkuu wa Wilaya (CCM) Iramba, Mkoani Singida.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka hiyo leo Machi 30 imekanusha na kueleza kuwa taarifa hiyo iliyokuwa ikisambazwa katika mtandao wa kijamii wa Facebook sio kweli.

Imeelezwa kuwa katika taarifa hiyo iliyosambazwa katika mtandao wa Facebook imeeleza kuwa Profesa. Kitila Mkumbo ambaye ni katibu mkuu Wizara ya maji Machi 20, 2019 aliwaita wajumbe 70 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Wilaya ya Iramba Mkoani Singida ambao pia wanatarajiwa kuwa wapiga kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu nchi nzima.

Aidha katika taarifa hiyo  iliyosambazwa katika mtandao wa kijamii wa Fcebook imeeleza kuwa katika mkutano huo Prof. Kitila Mkumbo alitoa hongo ya shilingi elfu hamsini kwa kila mjumbe kwa lengo la kuwashawishi ili waweze kumchagua pale muda wa uchaguzi utakapofika na kwamba mkutano huo ulisambaratishwa na TAKUKURU Mkoa wa Singida.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa TAKUKURU Mkoa wa Singida haikushiriki kwa namna yoyote ile katika tukio tajwa na wala haikuwa na taarifa ya uwepo wa kikao kama hicho Machi 29, 2020 katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida na kuwataka wananchi kufahamu kuwa TAKUKURU ni chombo kinachotambua majukumu yake na kinafanya majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.


Share:

LADHA YAKE TAMU HULETA MSISIMKO, FURAHIA JAMBO UBUYU





Share:

Breaking : IDADI YA WAGONJWA WA CORONA TANZANIA YAFIKIA 19


 Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa wa corona nchini Tanzania wamefikia 19, baada ya watano kuongezeka leo Jumatatu Machi 30, 2020.
Taarifa iliyotolewa na waziri huyo leo inaeleza kuwa wagonjwa hao watano walifanyiwa vipimo katika maabara kuu ya Taifa, “kati ya wagonjwa hawa, watatu ni kutoka Dar es Salaam na wawili kutoka Zanzibar ambao taarifa zao zimetolewa na Waziri wa Afya Zanzibar.”

“Hivyo sasa jumla ya wagonjwa wa corona ni 19 akiwemo mgonjwa mmoja aliyetolewa taarifa na Waziri wa Afya Zanzibar Machi 28, 2020.”

Kuhusu taarifa za wagonjwa wapya wa Dar es Salaam, Ummy amesema, “mwanaume mwenye miaka 29 Mtanzania alikutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi. Mwanamke mwenye miaka 21 Mtanzania ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.”

“Mwanaume mwenye umri wa miaka 49 Mtanzania ambaye pia ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.”




Share:

Rwanda Yaongoza Afrika Mashariki kwa Maambukizi ya Virusi Vya Corona....Waliombukizwa Hadi sasa ni 70

Rwanda imethibitisha visa 10 vipya vya maambukizi ya ugonjwa wa Corona  siku ya Jumapili na kufikisha 70 jumla ya watu wanaougua corona, Wizara ya afya Rwanda imetangaza.

Katika hotuba yake kwa taifa usiku wa Ijumaa Rais Paul Kagame alisema idadi hiyo itaendelea kuongezeka kwasababu wale waliotangamana na waathirika wanaendelea kutafutwa.

Katika visa vya hivi punde vya maambukizi, watu sita walitokea Dubai, wawili kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Nigeria na mwigine alikuwa amesafiri maeneo ya Afrika mashariki hivi karibunii, ilisema taarifa ya wizara ya afya nchini humo.

Rwanda inaongoza kwa visa vya maambukizi ya ugonjwa wa corona katika kanda ya Afrika Mashariki ikiiwa na wagonjwa 70, ikifuatiwa na Kenya 42, Uganda 33, Tanzania 14, huku Burundi na Sudan Kusini zikiwa hazijarekodi visa vyovyote vya maambukizi.


Share:

Idadi Ya Maambuki ya Corona Nchini Kenya Yafika 42


Watu wanne zaidi wameambukizwa virusi vya Corona nchini Kenya na kufikisha idadi ya wagonjwa kufikia 42, wakati huu serikali nchini humo ikiendelea kutekeleza amri ya watu kutotoka nje, ambayo imeathiri shughuli za biashara .

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema kuwa watatu walioambukizwa ni raia wa Marekani, Cameroon na Burkina Faso, huku mmoja akiwa raia wa Kenya.

Maambukizi matatu yameripotiwa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi na moja jijini Mombasa. watu 1,426 waliotangamana na ambao wanashukiwa kuambukizwa virusi hivyo wanatafutwa.

Hata hivyo wataalamu wa afya wanasema licha ya mikakati muhimu iliyotangazwa na Serikali kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, vita ya kuukabili itakuwa ngumu ikiwa wananchi hawataendelea kuelimishwa kuzingatia usafi na njia za kujikinga.

Kenya kwa sasa inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwatafuta watu waliotangamana na watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Hivi karibuni msemaji wa serikali, Cyrus Oguna, alitoa wito kwa watu ambao huenda walitangamana na wagonjwa walioambukizwa virusi hivyo kufika katika kituo cha afya kilicho karibu nao.


Share:

Marekani Yaendelea Kuongoza Kwa Maambuzi ya Virusi Vya Corona Duniani

Maambukizi ya kirusi cha corona yamepindukia 142,000 nchini Marekani na kulifanya taifa hilo kuongoza duniani, huku waliopoteza maisha wakipindukia 2,500.

Katika jimbo la New York pekee, watu zaidi ya 1,000 wameripotiwa kufa, ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu mgonjwa wa mwanzo kugundulika kwenye jimbo hilo.

Kufikia jioni ya jana, eneo la mjini la jimbo hilo lilitangaza kuwa vifo vimefikia 776, huku miji mingine ikitangaza vifo 250, na hivyo kuifanya idadi kamili ya waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi hicho kufikia 1,026.

Hayo yanakuja wakati Rais Donald Trump akitangaza kwamba huenda vifo vyote vitavyotokana na kirusi hicho vikapindukia 100,000 nchini Marekani. Trump ameongeza muda wa watu kujitenga ili kuepuka maambukizi mapya hadi tarehe 30 mwezi Aprili.

Muda wa awali uliowekwa ulikuwa wa wiki mbili, ambao unamalizika leo.


Share:

China Yatangaza Ushindi Dhidi Ya Virusi Vya Corona

China inasema kuna wagonjwa wapya 31 wa ugonjwa wa COVID-19 na vifo vinne hivi leo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Afya ya nchi hiyo. 

Miongoni mwa wagonjwa hao 31, thalathini walitoka nje ya nchi hiyo, na ni mmoja tu aliyeambukizwa katika jimbo la kaskazini magharibi la Gansu. 

Wanne waliofariki dunia ni kwenye jimbo la Hubei, chimbuko la maambukizi ya kirusi cha corona, ambalo hata hivyo halina mgonjwa mpya.

 Jimbo hilo lililokuwa kwenye marufuku ya kutotoka nje, limeanza kurejea kwenye maisha yake ya kawaida. 

"Maambukizi kutoka nje" ndicho kikwazo kikubwa kwa China kwa sasa, baada ya hapo jana Baraza lake la Taifa kutangaza kwamba kimsingi nchi hiyo imefanikiwa kuuzuwia ugonjwa wa COVID-19. 

Tangu kirusi hicho kianze kusambaa mwezi Disemba mwaka jana, watu 81,470 wameambukizwa nchini China pekee, ambako 3,304 wamepoteza maisha.

-DW


Share:

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA TPSF SALUM SHAMTE AFARIKI DUNIA


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)  na Mkurugenzi wa zamani wa Katani Limited Salum Shamte amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mkewe Mariam Shamte amethibitisha.


Share:

ZITTO KABWE ATAJA MAMBO 8 KUKABILIANA NA CORONA


Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ametoa mapendekezo manane kupitia barua aliyomwandikia Rais John Magufuli, kuhusu nini kifanyike katika kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa wa corona.


Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini, kwenye barua hiyo alitoa pia ushauri juu ya namna nzuri ya udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa huo, ambao umekuwa tishio katika nchi nyingi duniani.

Kwanza, Zitto alipendekeza kuwapo kwa umoja wa kitaifa ambao utawaweka Watanzania pamoja kwa vitendo hali itakayofanikisha kupambana na ugonjwa huo.

“Hakuna wakati nchi yetu inahitaji umoja kama wakati huu. Wewe kama mkuu wa nchi una wajibu mkubwa wa kuwaweka Watanzania pamoja kwa vitendo. Tukiwa wamoja tutaweza kupambana na corona na kushinda pamoja na ikibidi kushindwa tushindwe pamoja,” alisema Zitto na kuongeza:

“Corona haitambui itikadi zetu za vyama, dini zetu wala makabila yetu. Corona inaua mashekhe na makasisi, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wanadiplomasia na wanamichezo na mbaya zaidi inaua hata wataalamu wa afya kama madaktari na manesi. Nakusihi sana, uunganisha nchi yetu sasa bila kuchelewa,” alisema Zitto.

Pili, Zitto alipendekeza wataalamu kupewa nafasi katika kuongoza mapambano na kwamba viongozi kuepuka kutoa maeneo ya jumla.

“Ni muhimu sana sisi viongozi kuepuka kutoa maneno ya jumla ambayo yanawapa wananchi wetu matumaini hewa, hivyo kusababisha hatari zaidi. 

“Tutoe nafasi kwa wataalamu wa afya kutuongoza katika mapambano haya ya kudhibiti corona. Ni lazima sasa, maneno tunayoyasema kwa umma na maamuzi tunayoyachukua katika kudhibiti mlipuko huu yazingatie ushauri wa wataalamu ,” alisema Zitto.

Tatu, alipendekeza serikali kuweka nguvu kubwa kwenye kupima wananchi ili kuwatambua wenye maambukizi, kuwatenga wasiambukize wengine, kuwatibu na kuwafutilia maendeleo yao.

Zitto alisema kazi ya upimaji iwe kampeni endelevu na kwamba serikali itumie vipimo ilivyosaidiwa sambamba na kutumia fedha za dharura ambazo Bunge lilizipitisha kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kununua vipimo vingi zaidi ili kupima wananchi.

Nne, Zitto alipendekeza kuwapo na uwazi wa takwimu za maambukizi mapya, wagonjwa mahututi na vifo kwani suala hilo ni muhimu sana katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Tano, Zitto alipendekeza kuepukwe maelekezo yanayopinga na kueleza kuwa hatua zichukuliwe kusimamisha vikao vyote vya kiserikali ikiwamo Bunge na Mahakama.

“Serikali ilichukua hatua muafaka kufunga shule na vyuo kote nchini ili kuzuia maambukizi. Hata hivyo, tunatuma ujumbe gani kwa wananchi, na hasa watoto wetu wanapoona wao wamefunga shule, lakini viongozi wanahutubia makumi ya watu hadharani? Wanapata ujumbe gani wanapoona Bunge linaendelea na vikao?” Alisema Zitto.

Sita, alipendekeza mahabusi na wafungwa waachiliwe na warudi nyumbani ama kumalizia vifungo au kusubiri upelelezi wa kesi zao.

Saba, Zitto alipendekekeza kufungwa kwa mipaka ya nchi kwa muda ili kudhibiti maambukizi, na kwamba kwa kufanya hivyo kutasaidia kuzuia maambukizi zaidi.

“Ni lazima kuzuia msongamano wa watu kwenye huduma za usafiri wa umma kwa kuagiza vyombo vya usafiri vya Jeshi la Wananchi, Polisi na hata watu binafsi kutoa huduma ya usafiri wa umma kwa uangalifu mkubwa,” alisema Zitto.

Nane, Zitto alipendekeza kuundwa kwa timu ya wachumi waliobobea waliopo ndani na nje ya serikali watakaofanya uchambuzi wa kina wa hali ya uchumi wa nchi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.



Share:

Sita wajeruhiwa na fisi Shinyanga

Watu sita wa familia moja wakazi wa kijiji cha mwangalanga kata ya Samuye wilayani Shinyanga wamejeruhiwa kwa kung’atwa na fisi katika maeneo mbalimbali ya miili yao na ikidaiwa watu hao wamejeruhiwa na fisi huyo baada ya kumzingira kwa lengo la kumuua

Tukio hilo lilitokea Machi 27, saa 10 jioni, katika kijiji cha Mwangalanga wakati fisi huyo alipovamia kijiji hicho na wananchi kumzingira kwa kumpiga na kusababisha watu hao sita kujeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa juzi na Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Deborah Magiligimba, ilisema baada ya watu hao kujeruhiwa walikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Zengo Jitonja, Nkuba Deteba, Juma Salaganda, Limbu Mihambo, Dutu Mdese, na John Matanda.

"Watu hawa wakati wakiwa wamemzingira fisi huyo na kuanza kumshambulia, aliwang'ata sehemu mbalimbali za miili yao, majeruhi watano walipata majeraha madogo na wemeruhusiwa kutoka hospitali," alisema Magiligimba.

"Majeruhi mmoja Nzengo Jintonja, ambaye alijeruhiwa vibaya kwa kung'atwa mikononi na mdomoni, yeye alikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga na hali yake siyo mbaya sana," aliongeza.

Alisema fisi huyo ameshauawa na wananchi walioendelea kumshambulia kwa kumpiga.


Share:

New Video: Harmonize – Bed Room

New Video: Harmonize – Bed Room


Share:

Jiko La Mkaa Lasababishavifo Vya Watu Wanne Shinyanga

SALVATORY NTANDU
Wakazi wanne wa kitongoji cha Ngilimba ‘B’ kata ya Ulowa halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga wamefariki dunia baada ya kuvuta  hewa yenye sumu  iliyosababishwa na mkaa waliouwasha kwenye jiko na kisha kuliweka ndani ya nyumba yao ili kujikinga na baridi.

Akungumza na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 28 mwaka huu  ambapo wanafamilia hiyo waligundulika kupoteza Maisha ndani ya nyumba yao wakiwa wamelalala  baada ya kuvuta hewa yenye sumu.

Kamanda Magiligimba aliwataja waliofariki dunia ni pamoja Masanja Emmanuel (35) ambaye ni baba wa familia hiyo,  Mngole Masanja (25) mkewe, Holo Masanja,(05) na Matama Masanja (03) wote wakazi wa Ngilimba.

“Tukio hili limesababishwa na  mvua iliyonyesha Machi 27 iliyoambatana na  baridi kali ndipo marehemu hao waliamua kulala na  jiko la mkaa ndani ya nyumba yao na kusababisha mgandamizo wa hewa kuwa mdogo uliosababisha wavute hewa yenye  sumu ya carbon monoxide”,amesema  Magiligimba.

Miili ya marehemu hao imekabidhiwa ndugu zao kwa ajili ya taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa daktari.

Mwisho.


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger