Friday 1 March 2019

MKUU WA MKOA ATUA KIJIJI CHA KABALE KUKAMILISHA MAANDALIZI YA MAZISHI YA RUGE

Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jeneral Marco Gaguti amefika nyumbani kijijini kabale, Bukoba katika msiba wa Ruge Mutahaba ili kuungana na kamati ya maandalizi kwa ajili ya kukamilisha mipango ya mazishi.

Mwili wa Ruge tayari umeshawasili nchini ukitokea Afrika Kusini na Utazikwa Jumatatu March 4, 2019 
Share:

STAND UNITED WATAMBA KUTEMBEZA KICHAPO KWA SIMBA SC... 'SIMBA LAZIMA BHAKINDWE'


Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja

Klabu ya Stand United 'Chama la Wana' imetamba kutembeza kipigo kwa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Simba SC katika mchezo utakaopigwa Jumapili Machi 3,2019 katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga.

Akizungumza na Waandishi wa Habari,leo Ijumaa, Machi 1,2019, Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja amesema wamejiandaa vizuri kupeleka kilio kwa Wekundu wa Msimbazi 'Simba SC'.

Amesema wamepata wiki nzima ya mapumziko,uongozi na benchi la ufundi chini ya Mwalimu Athuman Bilal 'Bilo wa Bironga', wamekaa na kuangalia namna ya kupata pointi tatu kutoka kwa Simba SC.

"Mwalimu amerekebisha mapungufu yote yaliyokuwepo na bado tumepata nafasi ya kutizama mikanda ya mechi za Simba jinsi alivyocheza na wenzetu Lipuli FC,Azam FC tukaona mapungufu yaliyokuwepo na wenzetu wakapoteza, tumekubaliana ni namna gani tutaziba hayo mapungufu na sisi kuweza kufanya vizuri kupata hizo pointi",amesema Dkt. Maeja.

"Kwa mechi hii wananchi wa Shinyanga na wadau wasiwe na wasiwasi, Boko atakuwa bokoboko,Kagere kwetu ni kasamaki,hivyo kataliwa,halafu huyu Okwi mechi zote huwa hamalizi,huwa anaishia dakika 20,15 anavua viatu anaomba atoke,sasa huyu tutamwite Ong'wise (wa kwetu),kijana wa kwetu....

Wazee wa Shinyanga wamesema msiwe na wasiwasi kwamba Simba lazima Bhakindwe "Simba lazima washindwe" na vijana waseme Yes! Yes! kwa hiyo karibuni muangalie mechi nzuri",amesema Dkt. Maeja. 

Mashabiki na wapenzi wa Stand United wamesema wanafurahia kuona Mnyama Simba akifungwa naye asikie machungu ya kufungwa,wakiipa moyo Stand United kwamba ipo nyumbani hivyo ni lazima Simba alale.

"Viporo vya Simba vinaweza kuchacha au kuvila vizuri lakini kinachotakiwa ni mpira kuchezwa kwa ufundi,kila timu itumie dakika 90 vizuri, waamuzi wawe fair wazingatie sheria 17 na atakayetumia hizo dakika 90 basi ni halali yake",ameongeza.

Aidha ameishukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Vinywaji Jambo Food Products LTD Salum Hamis (Salum Mbuzi) maarufu Jambo ambaye ni mdhamini Mkuu wa Stand United kupitia kinywaji chake cha Jambo Cola kwa kuendelea kuwa pamoja na Stand United kuhakikisha wachezaji wanakula vizuri kambini na kusafiri vizuri lakini pia wadau,wapenzi na wanachama kwa kuendelea kuiunga mkono timu.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Share:

Picha : MWILI WA RUGE MUTAHABA WAWASILI DAR

Mwili wa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji Clouds Media Group, Ndugu Ruge Mutahaba umewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukitokea Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Aliyeongoza mapokezi ya Mwili wa Ruge Mutahaba ni Waziri January Makamba akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es aalaam pamoja na Mkurugenzi wa Clouds Media Group.
Gari lililobeba mwili wa marehemu Ruge Mutahaba likiwa linaondoka Airport kuelekea hospitali ya Lugalo.
Share:

ZITTO KABWE ASIKITIKA MAJAJI KUTOWAPATIA DHAMANA MBOWE NA MATIKO


Kiongozi wa Chama Cha ACT - Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe amesikitishwa na majaji kutotumia mamlaka yao katika kuwapatia dhamana Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Zitto Kabwe ametoa maoni yake hayo muda mfupi baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa za DPP na kwamba hazikuwa na mashiko.

Kesi hiyo iliyokuwa ikisimamiwa na Wakili upande wa utetezi, Prof. Abdullah Safari, Jopo la majaji limesema rufaa ya DPP haina mashiko na kwamba Jaji Sam Rumanyika alikuwa sahihi kukubali kusikiliza rufani ya kupinga kutenguliwa dhamana ya washtakiwa.

Zitto amesema, "Nimeridhika na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali rufaa za DPP dhidi ya uamuzi wa Jaji Rumanyika kutupilia mbali pingamizi zao. Hata hivyo nimesikitishwa sana na Majaji kutoamua kutumia mamlaka yao kutoa dhamana ilhali kuna ‘precedent’( historia) ya Jaji Luanda kwenye kesi ya Lema".

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018 baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo pamoja na viongozi wengne saba wa chama hicho.
Chanzo - EATV
Share:

MAREKANI YATANGAZA KUTOA MABILIONI YA FEDHA KUMSAKA MTOTO WA OSAMA BIN LADEN

Marekani imetangaza zawadi ya $1 milioni (sawa na 2,345,300,000 za Tanzania) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa mtoto wa kiume wa kiongozi wa Al-Qaeda, Osama Bin Laden.

Taarifa rasmi ya Serikali ya Marekani imeeleza kuwa Hamza Bin Laden amekabidhiwa jukumu la kuwa kiongozi wa Al-Qaeda na anapanga mashambulizi ya kigaidi.


“Serikali ya Marekani inatoa zawadi kwa taarifa kuhusu Hamza Bin Laden. Tunawahakikishia usiri mkubwa na uwezekano wa kuhamishwa eneo ulipo upo. Kama unazo taarifa, tafadhali wasiliana na ubalozi wa Marekani ulio karibu nawe,” tafsiri ya sehemu ya taarifa ya Marekani.


Taarifa za awali zinaeleza kuwa Hamza anaweza kuwa karibu na mipaka ya Afghanstan na Pakistani.


Hivi karibuni, alisambaza video na sauti zenye jumbe za kuwahamasisha wafuasi wa kundi hilo duniani kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani na marafiki wao wa Magharibi kwa lengo la kulipiza kisasi cha kifo cha baba yake.


Mwaka 2011, kikosi namba mbili cha makomando wa Marekani kilivamia maficho ya Osama Bin Laden katika mji wa Abbottabad nchini Pakistani na kumuua. Osama anatajwa kuagiza utekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 nchini Marekani ambayo yalisababisha vifo vya takribani watu 3,000.

Hamza Bin Laden ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hivi sasa, anadaiwa kuwa amemuoa binti wa Mohammed Atta, ambaye alihusika kuteka moja kati ya ndege za abiria na kugonga mnara wa jengo la Biashara (World Trade Center) jijini New York.


Barua ambazo zilipatikana kwenye nyumba ya Osama baada ya kuuawa, zinadaiwa kuonesha jinsi ambavyo alikuwa akimkubali na kumpa nafasi Hamza kama mtoto wake mpendwa zaidi na ambaye anaweza kuchukua jukumu la kuiongoza Al-Qaeda.


Osama ambaye ni mzaliwa wa Saudi Arabia alienda Afghanistan miaka ya 1980 ambapo alijiunga na kundi la Mujahideen lililokuwa linasaidiwa na Marekani kupigana na vikosi vya Soviet ambavyo vilikuwa vimeikalia ardhi ya Afghanistan.


Alianzisha taasisi kwa kwa ajili ya kuwasaidia watu waliokuwa wanajitolewa kuungana na Mujahideen kupigana kuikomboa ardhi ya Afghanistan, aliita taasisi hiyo ‘Al-Qaeda’. Mwaka 1989 aliondoka Afghanistan. Alirejea tena mwaka 1996 na kuanzisha kambi ya kutoa mafunzo ya kijeshi kwa maelfu ya wapiganaji wenye mlengo wa imani ya itikadi kali.


Baada ya muda, Al-Qaeda ilitangaza rasmi vita dhidi ya Marekani, Israel na washirika wao.
Share:

IGP SIRRO APANGUA PANGUA MAKAMANDA WA POLISI...RPC SHINYANGA ASUKUMWA MAKAO MAKUU


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro amefanya mabadiliko ya kiuongozi kwa maofisa wa jeshi hilo baada ya Rais John Magufuli kufanya uteuzi wa makamishna wapya.


Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi Mosi, IGP Sirro amewataja makamishna walioteuliwa na Rais Magufuli kuwa ni Charles Mkumbo ambaye anakwenda kuongoza kamisheni ya intelijensia na Liberatus Sabas ambaye anakuwa mkuu wa operesheni na mafunzo.

Wengine ni Leonard Lwabuzala ambaye ataongoza kamisheni ya fedha na logistics na Benedicto Wakulyamba ambaye anakuwa mkuu wa kamisheni ya utawala na menejimenti ya utumishi na Shaaban Mlai ambaye ataongoza kamisheni ya maabara ya uchunguzi wa kisayansi.

Mbali na makamishna hao, Sirro amefanya mabadiliko ya kiutawala kwa maofisa wa jeshi hilo; James Mushi ambaye alikuwa kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma anakuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi (CCP) Moshi wakati RPC wa Njombe, Renata Mzinga akirudishwa Makao Makuu.

Sirro amewataja makamanda wapya wa mikoa kuwa ni Amon Kakwale (RPC wa Temeke), Jonathan Shana (RPC Arusha), Marwa Mahiga (RPC Ruvuma), Salum Hamduni (RPC Njombe) na Zuberi Chembela (RPC Ilala).

Viongozi wengine waliohamishwa vituo vya kazi ni Mihayo Nsekela (ofisi ya operesheni na mafunzo), Simon Haule ambaye alikuwa RPC wa Shinyanga anarudishwa Makao Makuu na Yusuph Sarungi ambaye alikuwa RPC Songwe anakuwa mkuu wa kitengo cha kushughulikia wizi wa mifugo (SPU).

Benedict Mapugila ameteuliwa kuongoza kikosi cha bandari wakati Michael Marwa anapelekwa makao makuu Zanzibar. Sirro amesema Albert Nyamhanga na Nsato Marijani wanakwenda Idara ya Wakimbizi ambayo iko chini ya Idara ya Uhamiaji.

Na Peter Elias, Mwananchi 


Share:

WANAWAKE WASEMA MAFANIKIO CHANYA YANAHITAJI USHIRIKISHWAJI WA WANAWAKE

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsi (TGNP) Lilian Liundi 

Wanawake kutoka taasisi mbalimbali wamesema kuwa mafanikio ya kiuchumi, kifikra, kielimu na afya yanahitaji ushirikishwaji wa mwanamke ili yawe chanya.

Wakizungumza leo Ijumaa Machi mosi kwenye mkutano wa siku moja wa kujadili mafanikio yaliyopatikana baada ya miaka 25 ya mkutano wa Beijing.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsi (TGNP) Lilian Liundi amesema kuwa licha ya fursa nyingi kwa wanawake kufunguka bado ushirikishwaji kwenye baadhi ya mambo unahitaji msukumo.

"Changamoto zimepungua lakini unyanyasaji wa kijinsia, fursa za kumiliki mali, fursa za kukua kiuchumi bado zinahitaji msukumo wa wanawake," amesema.

Amefafanua ili kufikia mafanikio ikiwamo malengo ya Milenia ipo haja ya kuendelea kuwainua wanawake kielimu, kiuchumi na kuwapa nafasi ya kutoa maoni na mawazo yao kwenye maamuzi ya mambo yanayohusu nchi yao.

"Nafasi hizo zipo chache na zinawafikia wachache hususani waliopo mijini, hivyo ili kujenga uelewa kwa wanawake wote nchini ipo haja ya nafasi hizo za kutoa maoni, mawazo ushauri na kushiriki kwenye maamuzi zifike kila kona ya nchi," amesema Liundi.

Amesema kupitia mkutano huo watajadili misingi ya mkutano wa Beijing, ambapo muhimu lilikuwa ni kuweka usawa, kuondoa dhana potofu juu ya haki za mwanamke.

Kwa upande wa mwanzilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Marry Lusimbi amesema kuwa mkutano wa Beijing ni wa kukumbukwa kwa sababu umefungua fursa ya wanawake kudai haki zao popote walipo na kilichobaki ni kuhakikisha Serikali inakwenda nao pamoja ili kupata matokeo chanya katika mipango ya maendeleo.

Amesema kabla ya mkutano huo hakukuwa na nafasi ya mwanamke kujitokeza hadharani na kutetea jambo lolote linalohusu haki zake.

"Aliyefanya hivyo alionekana amekiuka dini, jamii, na asiyestahili kuolewa, lakini sasa harakati za kumkomboa mwanamke zinatambulika duniani kote," amesema na kuongeza.

"Wakati tunarudi Beijing Rais alikuwa Benjamini Mkapa, alipokea ripoti tuliyorudi nayo na mambo yaliyokuwemo yanafanyiwa kazi kisera, kibajeti , lakini kuna wenzetu ikiwamo Kenya wakati huo Rais alikuwa Moi aliwaambia Beijing yao waiache huko huko uwanja wa ndege, hivyo ilikuwa bahati kwetu na mafanikio yanaonekana kwenye baadhi ya maeneo, wanawake wanaweza kupaza sauti na wakasikilizwa," amesema Lusimbi.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo waliyajadili na sasa yamefanyiwa kazi hadi kwenye bajeti ni pamoja na suala la usawa maarufu 50 kwa 50.

Kwa upande wa Mary Ndaro kutoka Care International amesema kuwa wanawake ndiyo wazalishaji wakuu hivyo wasiposhirikishwa mpango wa 20/25 utabaki ni mpango tu na hautatekelezeka.

Amesema mwanamke akishirikishwa kwenye jambo hususani la kitaifa uelewa na utekekezaji kwenye jamii unakuwa mkubwa na wenye ufanisi kwa sababu wapo kwenye nyanja zote ikiwamo kuijenga jamii.

Na Kalunde Jamal, Mwananchi 
Share:

UTAFITI WA MUHAS WAONYESHA CHANJO DHIDI YA VVU NI SALAMA


Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia MUHAS, Eligius Lyamuya akiwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) iliyofanyiwa majaribio katika maeneo mbali mbali ya nchini Tanzania na Msumbiji wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam. Picha zote na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Wageni waalikwa na wafunzi wa Chuo Kikuu MUHAS wakifuatilia.
Wageni waalikwa na wafunzi wa Chuo Kikuu MUHAS wakifuatilia.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof Andrea Barnabas Pembe akitoa neno la ufunguzi wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Muhadhara huo, Prof. Kisali Pallangyo akiendesha muhadhara wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia wa Chuo cha Afya St. Joseph, Fred Mhalu akichangia mada wakati wa kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Prof. Said Aboud na Dkt Edith Tarimo.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi akitoa ufafanuzi wa jambo.
Kamishna Msaidizi wa Polisi na Maganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ACP Dkt Charles Msenga akitoa mchango wake katika kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa akifunga kongamano la Kisanyansi la Kitafiti lililofanyika jijini Dar es Salaam lililokuwa na lengo la kuwasilisha matokeo ya utafiti wa Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kamishna msaidizi wa Polisi na Maganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam ACP Dkt Charles Msenga (kulia) akiteta jambo na Dkt Patricia Munseri wa MUHAS.

Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.

Chanjo dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) inayofanyiwa majaribio nchini Tanzania ni salama na ina uwezo wa kuufanya mwili kutengeneza viashiria vya kinga.

Hata hivyo hiyo haimaanishi chanjo hiyo ni kinga dhidi ya Maambukizi ya Virusi (VVU) hivyo, matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), yamebainisha.

Akiwasilisha matokeo hayo, Profesa wa Mikrobiolojia na Immunolojia MUHAS, Eligius Lyamuya, amesema chanjo hiyo iliyofanyiwa majaribio imetengenezwa nchini Sweden na wataalam wenzao ambao wanashirikiana nao katika masuala ya tafiti.

"Tumeifanyia utafiti chanjo hii tuliangalia iwapo ni salama na iwapo ina uwezo wa kuchangamsha ile kinga ya mwili kutengeneza viashiria vya kinga na iwapo ina uwezo wa kutengeneza chembe chembe hai za mwili.

"Au uwezo wa kutengeneza molecular mbalimbali ambazo zinaashiria hii inaweza kuwa zinahusika katika kinga dhidi ya chanjo ambayo imetolewa.

" Hivyo, tumebaini chanjo hii ni salama na wote waliochanjwa hakuna ambaye amepata madhara yoyote hadi sasa wako vizuri," alisema.

Aliongeza "Jambo la pili ni kwamba tuna ushahidi kulingana na tafiti yetu chanjo hii inachangamsha ile kinga ya mwili kutengeneza viashiria vya kinga.

"Lakini hivi viashiria vya kinga vinavyotengenezwa haina maana kwamba ndiyo kinga yenyewe dhidi ya maambukizi ya VVU, hapana hivi ni viashiria tu vitahitaji kitu kingine zaidi kuona kama vina uwezo wa kupigana na vile virusi au la!," alisema.

Amesema katika kutengeneza chanjo hiyo wataalam wenzao wa Sweden waliangalia pia iwapo itafaa kutumika katika mazingira yetu au la!

"Tulikubaliana lazima ifae katika mazingira yetu kwa maana kwamba itakapotengenezwa huko siku zijazo kuwe na uwezekano wa kukinga dhidi ya virusi vya ukimwi ambavyo vipo katika mazingira yetu maana kuna aina nyingi ya virusi," amesema.

Amesema matokeo hayo yana maana kubwa kwamba bado wanaweza kuendeleza tafiti hizo kwa kushirikisha wahusika (sampuli) wengi zaidi.

"Katika hatua ya kwanza tulihusisha watu, wahusika walikuwa 60, lakini walioweza kupata chanjo zote tatu walikuwa 56 na walioweza kupata chanjo zote tatu na nyingine mbili za ziada walikuwa 42.

"Hii ina maana kuna ambao waliachia kwa sababu zao binafsi lakini kwa sababu ushiriki ni wa hiari hatuwezi kuuliza mtu kwa nini hakushiriki kupata chanjo mwanzo hadi mwisho," alisema.

Akizungumza, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi amesema matokeo ya utafiti huo yameonesha wazi namna MUHAS ilivyofanya kazi kubwa kuunga mkono jitihada za kidunia katika kutafuta chanjo dhidi ya Ukimwi.

"Wizara tunaunga mkono juhudi hizi kwa sababu dunia inamaanisha tunaweza kufikia hatua ya kupata chanjo itakayofanya kazi vizuri, iliyo salama na kwa bei nafuu ambayo itasaidia mno katika kudhibiti maambukizi ya Ukimwi," alisema.

Ameongeza "Kimsingi, yamefanyika majaribio mengi, kizuri katika yote haya chanjo zimeonekana ni salama na zina uwezo wa kufanya mwili kutengeneza vichocheo vya kinga.

"Sasa chuo kitajikita kutafiti iwapo itakuwa na uwezo wa kukinga watu kutopata maambukizi ya ukimwi," amesisitiza Profesa Kambi.

Share:

JAMAA AJIUA KWA KUGONGWA BASI BAADA YA KUGOMBANA NA MPENZI WAKE

Jamaa mmoja mwenye umri wa makamo ameripotiwa kufariki dunia baada ya kugongwa na basi lililokuwa likiendeshwa kwa kasi kutoka mjini Kisumu kuelekea Nairobi nchini Kenya.

 Tukio hilo limetokea Alhamisi Februari 28,2019 eneo la Kachok katika barabara kuu ya Kisumu kuelekea Nairobi. 

Inasemekana jamaa huyo alifanya kitendo hicho saa chache tu baada ya kugombana na mpenziwe ambapo inasemekana kumfumania mpenziwe akifanya mapenzi na rafiki wake wa karibu.

Aliyeshuhudia ajali hiyo alisema marehemu alijirusha katikati ya barabara kutoka kwenye daraja lililo karibu na shule ya upili Lions na kukanyagwa vibaya na basi lililokuwa likiendesha kwa kasi. 

 Inasemekana marehemu alikuwa amegombana na mpenzi wake saa chache kabla ya kutekeleza kitendo hicho.

 Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga. 

 Kisa hiki kinatokea siku chache tu baada ya kingine sawa kuripotiwa mjini Naivasha eneo la Kayole ambapo jamaa mmoja pia alijirusha barabarani na kugongwa na gari lililomuua papo hapo.

Share:

MKUBWA FELLA AWAJIA JUU WANAOMTUKANA MAREHEMU RUGE

Mtendaji Mkuu wa Mkubwa na Wanawe Youth Organization Mkubwa Fella ameamua kufunguka kuhusiana na ukaribu aliokuwa nao na Marehemu Ruge Mutahaba pamoja na taarifa za msiba kumuumiza kutokana na wawili kujuana tokea mwaka 1995 na kusaidiana vitu vingi.

Fella ameongeza na kusema kuwa watu kwenye mitandao inabidi waache kutukana kwa sababu Marehemu Ruge ana mchango mkubwa kwenye maisha ya muziki na walikutana hata kabla ya Ruge kwenda kwenye matibabu na hivyo cha muhimu ni kumuombea.

“Najua tumeumia wengi na kila mtu anajua uchungu wa kuondokewa mfano mie najua uchungu wa kufiwa na baba, mama mpaka mtoto machungu yote nimepitia kweli msiba unauma alafu kati ya watu wa karibu na Ruge kati ya watu wake 10 sikosi kwani alijua umuhimu wangu nami nilijua umuhimu wake sasa kwa msiba wa mwanangu bosi wangu nimeumia ila nami nipo kwenye ibada napitia naumwa ila naona wapenda ukolofi wanatukana sijuhi wao wanaitaji nifanyeje chengine


“Namini mie na marehemu tunajuana kuliko wewe unaepita kwenye ukurasa kutukana watu unajua vita ngapi tulipigana kuusogeza mziki huu na tasnia hii nimejuana na Ruge 1995 mpaka leo sasa usilete utashi wa biashara kutukana watu mie nilipata bahati kuagwa na brother na wakati anatarajia kwenda kwenye matibabu kabla ajazidiwa yeye ndio alinambia kijana wako mmoja kwenye ya moto atakusumbua ila kuwa makini tena akanisifu najua moyo wako mpana utashinda


“Kuna siku alinambia Fella nikirudi salama napenda tukae tujue tunajengaje mnara timilifu sasa wewe mwenye account yako ya kutukana watu sio vizuri msiba ni mkubwa alafu kulia kila mtu anakilio chake sasa usikae ukaona unavyo lia wewe na mwengine uwe sawa lakini najua yatapita ila nakumbuka baba yangu alifariki 2006 siku iyo ilikuwa Fiesta Arusha nimetoka home alfajiri natua Arusha napigiwa mzee kafariki nakumbuka Boss Kusaga na Ruge walinambia usiuzunike siku hii ila sema asante


“Mwenyezi Mungu kwa kunipatia ili kuiona siku ya mwisho ya baba sasa kama nilipewa mawaidha aya na nikashinda sasa ili la msiba wa boss Ruge muhimu naona ni kumuombea kwa mwenyezi Mungu amuweke pahala pastahiki. nasi tunae subiri time yetu tuwaombee dua marehemu wetu wote tuseme Inshaallah pia instar iwe kipasha habari isiwe ibada eti umu kama ndio mwenyezi Mungu anakagua. kweli wakati mgumu ila tuikaribishe subraaaaa na Inshaallah mwenyezi Mungu tuongoze Amen"
Advertisement
Share:

MCHUNGAJI ALIYEFUFUA MTU ATAKIWA KUMFUFUA MANDELA


Baada ya sakata lake la kumfufua mtu kutinga kwenye vyombo vya habari na kuzua gumzo katika bara zima la Afrika, Mchungaji Alph Lukau sasa ametakiwa na mchungaji mwenzake kumfufua Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Nelson Mandela.

Mchungaji huyo wa kanisa la Alleluia Ministry la Afrika Kusini, ametakiwa kufanya hivyo na mchungaji mwenzake anayejulikana kwa jina la Paseka Mboro Motsoeneng maarufu kama Pastor Mboro, baada ya kwenda kanisani kwake kumtaka atoke nje na kulitolea majibu suala hilo lililoleta mtafaruku kwenye imani.

“Kwa nini unakimbia kama siko sahihi!?, nataka ujisalimishe na uombe radhi. Naweza kuuona uongozi wa kanisa!?. Labda naweza kuombewa na mimi, nataka kumuita mchungaji na tuende kwenye kaburi la Mandela ukamfufue”, amesema Pastor Mboro kwa hisia huku waumini wa kanisa hilo wakitawanyika.

Licha ya maneno hayo huku watu wakiwa wamejaa nje ya kanisa lake, mchungaji Lukau hakutaka kujitokeza, na kuzidi kupandisha hasira za waliofika kanisani hapo, huku wakimtuhumu kuidhalilisha imani ya dini ya Kikristo, na kwamba anadanganya umma kwa kutumia jina la Mungu.
Mchungaji Mboro akiwa nje ya kanisa la Mchungaji Alph Lukau akimuomba atoke nje na kuomba radhi kwa kudhalilisha dini.
Share:

DUDU BAYA AACHIWA KWA DHAMANA POLISI


 Hatimaye Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limemuachia kwa dhamana msanii wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini maarufu kwa jina la Dudu Baya, baada ya kumshilikia kwa saa kadhaa.

Dudu Baya alikamatwa juzi Jumatano, Februari 27 usiku nyumbani kwake Mbezi na kufikishwa katika kituo cha Polisi Oystebay kwa ajili ya mahojiano.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Waziri wa Habari na Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuagiza Jeshi la Polisi na Baraza la Sanaa la Taifa(Basata) kumchukulia hatua mwanamuziki huyo kwa makosa ya kumdhihaki, aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Akizungumza na Mwananchi leo, Ijumaa Machi 1, 2019, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mussa Taibu amesema walimwachia msanii huyo jana Alhamisi, Februari 28 saa 9:00 mchana baada ya kumaliza kumuhoji.

Kamanda Taibu amesema pamoja na kumuachia huko bado upelelezi unaendelea dhidi yake.

Kamanda huyo alipotakiwa kusema ni lini hasa msanii huyo atapaswa kurudi tena kituoni hapo, amesema suala hilo ameiachia ofisi ya upelelezi na kuahidi kulitolea majibu badaye.

"Unajua kwa sasa jambo hili lipo katika ofisi ya upelelezi wao ndio wanajua ni lini wamempangia arudi, ila ninachojua ni kwamba upelelezi dhidi ya msanii huyo unaendelea," amesema Kamanda Taibu.

Dudu Baya alikamatwa na polisi na kufunguliwa jalada la kesi lenye namba OB/RB/2029/2019 la matumizi mabaya ya mitandao kutokana na kitendo chake hicho cha mara kadha kumkashifu marehemu Ruge kabla na baada ya kufariki kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa kujirekodi video kwa nyakati tofauti.

Na Nasra Abdallah, Mwananchi
Share:

RAIS MAGUFULI ATOA NDEGE KUSAFIRISHA WANAOTAKA KWENDA KUMZIKA RUGE


Rais John Magufuli ametoa ndege ya Serikali kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa marehemu Ruge Mutahaba utakaopelekwa Bukoba kwa ajili ya kuzika.



Msemaji wa Familia ya Mutahaba, Raymond Kashasha amesema hayo leo Ijumaa, Machi 1,2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Ruge anatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Kiziru wilayani Bukoba mkoani Kagera na atasafirishwa kutokea Dar es Salaam siku ya Jumapili, Machi 3,2019.

Pia ametoa ndege ya Air Tanzania kwa ajili ya watu wanaotaka kwenda kumzika Ruge ambayo itaondoka Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Februari 4 asubuhi kwa gharama ya Sh 600,000 kwenda na kurudi.

Na  Hellen Hartley, Mwananchi
ANGALIA VIDEO HAPA
Share:

BASATA YASITISHA USAJILI WA MSANII DUDUBAYA

Baraza la Sanaa la Taifa(BASATA) limesitisha usajili wa Msanii Godfrey Tumaini(Dudubaya),kuanzia jana Alhamisi, 28 Feb 2019 . 

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya msanii huyo kukamatwa na jeshi la polisi, kutokana na kutoa kauli zisizofaa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Ruge Mutahaba
Share:

FREEMAN MBOWE NA ESTHER MATIKO WASHINDA RUFAA YA DHAMANA YAO DHIDI DPP

Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali pingamizi la Serikali kupinga Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko kusikilizwa shauri lao la kuomba kupewa dhamana katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.

Hivyo kesi ya Mh. Mbowe na Matiko inarudi Mahakama kuu kwa ajili ya kusikilizwa kama ilikuwa halali kwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu kufuta dhamana zao au hapana.

Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Wawili hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika.

Hata hivyo, baada ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Sam Rumanyika kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Upande wa serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi ulidai kuwa wamekata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu.
Share:

MBUNGE WA CHADEMA ALAZWA KCMC

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA) amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, ambapo alifikishwa Februari 27 mwaka huu. Mbunge huyo anasumbuliwa na shinikizo la damu.

Katibu wa Chadema, Mkoa wa Kilimanjaro Basili Lema amethibitisha kulazwa kwa Mbunge huyo.
Share:

KESI YA HOUSE BOY KUDAIWA KUMUUA HOUSE GIRL YAUNGURUMA

Shahidi wa pili katika kesi ya mauaji ya mfanyakazi wa ndani wa kike wa Jaji mstaafu, Engela Kileo anayedaiwa kuuawa na mfanyakazi mwenzake wa ndani wa kiume, ameileza Mahakama kilichowasukuma kufanya upekuzi chumbani kwa mshtakiwa na kukuta mabegi ya nguo za marehemu na simu.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 96 ya mwaka 2016, mshtakiwa Philemon Laizer anadaiwa kumuua Lucy Maina kwa kukusudia. Philemon mwenyeji wa Arusha na Lucy ambaye alikuwa raia wa Kenya walikuwa wafanyakazi nyumbani kwa Jaji Kileo.

Philemon anadaiwa kumuua Lucy Juni 8, 2013 usiku wa manane nje kidogo ya nyumba hiyo waliyokuwa wakifanya kazi Mikocheni B jijini Dar es Salaam kutokana na sababu za kimapenzi na kisha kuutupa mwili kichakani.

Shahidi huyo ambaye kwa sasa ni mkuu wa upelelezi mkoa wa Kigoma (RCO), mrakibu mwandamizi wa polisi, Mark Njela aliieleza:“Tulipotaka kwenda chumbani kwake kwanza alikataa Jaji (Kileo) ndio akamwambia wape nafasi. Tulipoingia tulikuta vitu mbalimbali. Kulikuwa na mabegi mawili ya nguo na mfuko wa nailoni yakiwa na nguo, viatu na simu ya SamSung vikiwa uvunguni mwa kitanda.”

“Tulipomuuliza mtuhumiwa vitu hivyo vilifikaje chumbani mwake baada ya kuvuta pumzi ndefu sana akakiri kwamba ni amehusika na mauaji hayo.”

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Jumatatu iliyopita na Jaji Yose Mlyambina katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam baada ya kimya cha takriban miaka sita.

Na James Magai, Mwananchi 
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger