Thursday 29 December 2016

Bodi ya Mikopo yaja na mbinu nyingine ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.

Bodi hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.

Pamoja na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB, na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30 walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.

“Tumeamua kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.

Aidha, alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado haitoshelezi.

Alisema bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu, hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa hiyo ya kujisalimisha.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.

Alisema utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi, kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda muafaka uliowekwa kisheria.

Badru alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo, imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na kutafuta ajira.

Aidha, alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya mishahara yao hadi asilimia 15.

“Tunawashukuru sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.

Alisema ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kupitia marekebisho hayo ya sheria.

“Tumeunda kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha michango hiyo kwa bodi,” alisema.

Alisema waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao, wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.

“Lakini pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato, yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.

Halikadhalika, Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira, ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila mwezi.

Akizungumzia mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha, yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni nane.

Alisema tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na wengine wakiyapunguza.

Hadi sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva, inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140 pekee ndio zimelipwa.

Kwa mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa wanafunzi hao.

Jumla ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria kuisha.
Share:

Hapi Aishika Pabaya Kampuni Ya ZanteL,Yalipa Mapato Zaidi Ya Milioni 687 Ndani Ya Siku 7 Ilizopewa

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Zantel Tanzania imelipa zaidi ya Sh milioni 687 baada ya kupewa siku saba na halmashauri hiyo iwe imelipa fedha hizo ambazo zilikuwa za kodi ya pango inazodaiwa na manispaa hiyo.

Fedha hizo zililipwa Desemba 21 na mkataba huo wa zamani unaisha Januari mwakani ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema wanaandaa mpya wenye viwango vya malipo vya sasa.

Aidha halmashauri hiyo imeamua kuelekeza fedha hizo ambayo ni sh 687,931,040 katika ujenzi wa vyumba vya madarasa 40 katika halmashauri hiyo kwamba kama itaonekana inawezekana kujenga shule nyingine mpya ya sekondari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Hapi alisema fedha hizo zimelipwa baada ofisi yake kubaini mchezo mchafu uliokuwa umefanywa na watendaji wa halmashauri yake waliokuwepo huko nyuma ambao walificha mkataba kati yake na Zantel.

Aidha aliipongeza Zantel kwa kutii maagizo waliyopewa na kulipa fedha hizo na tayari wamepewa risiti kuonesha kupokea fedha hizo na kwamba watu wote waliohusika katika jambo hilo watachukuliwa hatua za kisheria. 
Alisema baada ya malipo hayo, ameelekeza Manispaa kutumia fedha zote hizo kujenga vyumba vya madarasa katika halmashauri hiyo.

“Takwimu zinaonesha mwaka huu watoto 19,000 walifaulu katika Halmashauri ya Kinondoni waliochaguli kujiunga na Sekondari ni 12,889 na hadi sasa wanafunzi 3,169 hawajapata nafasi katika shule zetu kwasababu ya ufinyu wa madarasa,” alisema Hapi.
Share:

Waziri Mkuu Achangia Mabati Ujenzi Wa Zahanati

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahimiza wakazi wa vijiji saba wilayani Ruangwa waharakishe kufyatua matofali ili waanze ujenzi wa zahanati na yeye atawachangia mabati.

Ametoa ahadi hizo jana (Jumatano, Desemba 28, 2016) wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi na Chibula na viongozi wa wilaya ya Ruangwa, mkoa wa Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. 
Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.Alisema sera ya Serikali ni kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na kwamba umefika wakati wa kuanza kutekeleza kaulimbiu ya jimbo hilo inayosema “Ruangwa kwa maendeleo, inawezekana.”

Katika kuhimiza ujenzi wa zahanati hizo, alichangia mabati kati ya 50 na 150 kwa kila kijiji na akawahimiza wahakikishe wanakamilisha mapema ujenzi wa maboma ili aweze kutimiza ahadi yake ya mabati.

Alisema katika awamu iliyopita, alikazania sana suala la elimu kwa kusimamia ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa kwenye shule ambazo hazikuwa na madarasa ya kutosha. Pia alisimamia ukarabati wa majengo chakavu katika baadhi ya shule.

“Kuanzia awamu hii na miaka minne iliyobakia, mkakati wangu ni kusimamia upatikanaji wa maji safi na suala la kuboresha sekta ya afya katika jimbo zima nikishirikiana na uongozi wa Halmashauri yetu,” alisema.
Pia alimwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Japhet Simeo ahakikishe anawasiliana na viongozi wa vijiji hivyo ili wapatiwe michoro ya ramani zilizoidhinishwa na Wizara ya Afya.

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa kampuni ya Umemejua ya Baraka Solar Specialist, Bw. Ansi Mmasi alisema atajitolea kuweka mfumo wa umemejua wa watts 300 pamoja na nyaya zake kwenye zahanati inayotaka kujengwa kwenye kijiji cha Namilema.
Alisema anaishukuru kwa kuwapa kazi makandarasi wazawa na akawataka wakandarasi wenzake watumie vifaa bora na imara pindi wanapopewa kazi ya kutoa huduma na taasisi mbalimbali ikiwemo halmashauri na idara za Serikali.

“Tujitahidi kufanya kazi hizi kwa weledi na tutumie vifaa bora na imara ili watu wanaotarajia huduma zetu waweze kuridhika na kuendelea kuwa na umani na wakandarasi wazawa kwamba tunaweza kufanya kazi nzuri na zenye ubora unaotakiwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Wanyumbani Construction, Bw. Fakihi J. Bakili alisema atachangia mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Namilema. Pia alichangia mifuko 100 kwenye zahanati ya kijiji cha Manokwe na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Chikundi.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Share:

Watu 7 Wafikishwa Mahakamani kwa kumchoma mkuki mdomoni mkulima

POLISI mkoani Morogoro imewafikisha mahakamani watu saba kati ya 12, kujibu tuhuma za kumjeruhi kwa kumchoma mkuki mdomoni hadi kutokea shingoni, Augustino Mtitu (35).

Walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa huku wengine watano, wote wakazi wa kitongoji cha Upangwa wilayani Kilosa wakisubiri kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema jana alipokuwa anazungumzia msako uliofanywa na polisi na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao baada ya kutokea kwa tukio hilo Desemba 25, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi eneo la kitongoji cha Upangwa, Kijiji cha Dodoma Isanga, Kata na Tarafa ya Masanze wilayani Kilosa.

Kamanda Matei alisema katika msako huo, watu 12 walikamatwa na saba kati yao tayari wamefikishwa mahakamani. Wengine watano watafikisha mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi.

Hata hivyo, Kamanda huyo aliwataja majeruhi wa tukio hilo mbali na Mtitu ambaye bado anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, kuwa ni George Andrew (68) aliyejeruhiwa kichwani.

Wengine ni Yohana Wisa (26) aliyejeruhiwa mkono wa kulia, Mathayo Elia (34) aliyejeruhiwa kichwani na bega la kushoto, Josephat Mtitu (55) aliyejeruhiwa begani na shavuni na mwingine ni Paulo Thomas (56) aliyejeruhiwa mbavu na mkono wa kushoto.

Wote ni wakazi wa kijiji cha Dodoma Isanga na wanaendelea vizuri. Hivi karibuni, baadhi ya wafugaji wa jamii ya kimasai waliwashambulia kwa silaha za jadi na kuwajeruhi watu sita akiwemo Mtitu mara baada ya kukamata mifugo ya mtu mmoja aitwaye Ngoyoni Kimang’ati, iliyokuwa ikiharibu mahindi shambani.
Share:

Mapya Yaibuka Sakata la Kijana Aliyefariki Baada ya Nyoka wake Kuuawa na Wananchi

Share:

Mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya yaongoza kwa maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI

Kutokana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kupungua kwa asilimia 50 duniani kote na kupelekea watu milioni 2.1 tu kuambukizwa Virusi vya Ukimwi katika mwaka 2015,kumeibua matumaini mapya ya kuwa na watu wasio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko aliwaambia waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam kuwa, nchini Tanzania maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi nayo yameshuka kwa asilimia 20 ambapo watu 54,000 wameambukizwa virusi hivyo kwa mwaka 2015 pekee.

Dkt. Maboko alisema, Ukimwi bado ni janga kubwa duniani na taifa kwa ujumla huku akitaja kundi la wanawake kuwa ndilo lina kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU huku mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya ukiwa na kiwango cha juu cha maambukizi hayo kitaifa.

Aidha, alisema serikali imejiwekea mikakati kuhakikisha kuwa waliogundulika kuwa wameathirika wanaanzishiwa dawa, kuhimiza matumizi ya mpira wa kiume, kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 29 na kutoa elimu kwa wanawake wanaojihusisha na ngono, kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Share:

Wassira akimbilia Mahakama ya Rufaa kumpinga Bulaya

WAZIRI mwandamizi wa serikali ya Tanzania kwa awamu nne za uongozi, Stephen Masato Wassira, kupitia kwa wafuasi wake watatu, amekata rufaa Mahakama ya Rufaa, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kuhalalisha ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema).

Wassira (71 ) alikuwa waziri kwa mara ya kwanza tangu Desemba 07, 1973 akiwa naibu waziri wa Kilimo na ameendelea kuwa kiongozi mwandamizi wakati wa serikali ya Mwalimu Julius Nyerere, akarithiwa wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi, baadaye Rais Benjamin Mkapa na hatimaye uongozi wa awamu ya nne wa Rais Jakaya Kikwete.

Tayari wafuasi hao wa Wassira; Magambo Masato, Matwiga Matwiga na Ascetic Malagaila, wamefungua kesi hiyo na imesajiliwa katika ofisi za mahakama ya rufaa jijini Mwanza tarehe 16 Desemba, 2016 na itakuwa ni kesi ya rufaa namba 199 ya mwaka 2016.

Katika rufaa hiyo iliyoandikwa na wakili wao, Constatine Mutalemwa, wametoa sababu kadhaa kama hoja zao za kukata rufaa.

Kwanza, wanadai kwamba jaji hakuzingatia makosa yaliyofanyika baada ya zoezi la kupiga kura.

Pili, Wassira au wakala wake wanadai hakuitwa kwenye majumuisho kujulishwa siku, mahali wanafanyia majumuisho.

Tatu, wanadai kuwa jaji hakutilia maanani kesi zinazofanana na hii zilizotolewa kama mfano mahakamani.

Nne, Jaji alikosea kutoa uamuzi kwa misingi ya maoni binafsi badala ya kuzingatia mambo ya maana.

Wanadai kuwa jaji alisema wananchi wa Bunda ni maskini waachwe wafanye shughuli za maendeleo kwa sasa.

Tano, wanadai jaji alikosea kuamua kuhusu sheria ya viapo na matamko iliyotajwa katika kanuni za kuendesha kesi za uchaguzi.

Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilitoa uamuzi wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliompa ushindi Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) dhidi ya Stephen Wassira (CCM).

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi ilifunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, lakini ilikuwa inasikilizwa mjini Musoma, mkoani Mara.

Mahakama hiyo ilieleza kutoridhishwa na ushahidi wa kupinga matokeo hayo uliowasilishwa na upande wa walalamikaji, hivyo ikamthibitisha Bulaya kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.

Kesi ya kupinga matokeo hayo ilifunguliwa na wafuasi wa Wassira ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuondolewa kupitia uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Katika kesi ya msingi, walalamikaji ambao ni wakazi wa Bunda walidai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kwakuwa uligubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanaemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura visivyo halali.

Katika kesi hiyo, Bulaya alitetewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu.
Credit: FikraPevu
Share:

Bodi ya Mikopo yawatosa Watanzania wanaosoma China

Watanzania waliopata ufadhili wa kusoma nchini China, hawatapata mikopo baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwaondoa kwenye orodha ya wanufaika. 
Taarifa iliyotolewa na HESLB, ikijibu Ubalozi wa Tanzania nchini China, kuhusu madai ya kuchelewa kwa fedha za mikopo kwa wanafunzi wanaosoma nchini humo imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maelekezo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwamba wanafunzi wote wanaopata ufadhili kutoka nchi rafiki watajitegemea ikiwamo gharama za tiketi za ndege.

Barua hiyo ya Desemba 20, 2016 iliyomnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul Razaq Badru inaeleza kuwa mwaka huu wanafunzi hao hawatanufaika na mikopo kama ilivyokuwa ikitolewa miaka ya nyuma.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari, Badru aliitambua barua hiyo huku akisita kutolea ufafanuzi wake kwa madai ilikuwa ni majibu kwa wanafunzi hao wa China.

Hata hivyo, alisema endapo kutakuwa na madai kutoka kwa wanafunzi hao watalazimika kutolea ufafanuzi.

Akizungumzia suala hilo Naibu Waziri Elimu, Stella Manyanya alisema ni hekima zaidi kuangalia au kusaidia wanafunzi wa ndani wasiokuwa nacho kuliko wanaopata ufadhili wa nje ya nchi.
Share:

MAGAZETI YA LEO ALHAMISI DEC TAREHE 29.12.2016


Share:

Wednesday 28 December 2016

SEKRETARIETI YA AJIRA DAR IMEFAFANUA TAARIFA KUHUSU KUFUTWA KWA AJIRA SERIKALINI WALIOFAULU USAILI

 Image result for SERIKALI YA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA



Mnamo tarehe 26 na 27 Desemba, 2016 baadhi ya mitandao ya kijamii imeandika taarifa zenye nia ya kupotosha Umma ambazo Sekretarieti ya Ajira inapenda kuzitolea ufafanuzi kama ifuatavyo;-
1. Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa ufafanuzi kufuatia hoja iliyoandikwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii ya tarehe 27 Desemba, 2016 zenye vichwa vya habari vinavyosomeka “Waliofaulu usaili ajira serikalini kufutwa” na “Taarifa kwa waliokuwa wakisubiri kupangiwa vituo vya kazi kabla ya ajira kusitishwa serikalini” zikidaiwa kutolewa na Taasisi hii katika majibu ya hoja za mwezi Novemba, 2016 katika utaratibu wake wa kujibu hoja za kila mwezi kama ifuatavyo;- 
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Sekretarieti ya Ajira tangu mwezi Juni, 2016 Serikali  ilipositisha  Ajira  hapakuwa na orodha ya waombaji kazi waliokuwa wakisubiri matokeo ya usaili, kwa kuwa usaili wa mwisho ulioendeshwa na Sekretarieti ya Ajira ulifanyika mwezi Mei, 2016 na waombaji waliofaulu walipangiwa vituo vya kazi kwa idaidi ya nafasi zilizokuwepo.
Aidha, kwa wale ambao walifaulu na hawakuweza kupangiwa vituo vya kazi  kutokana na kukosekana kwa nafasi zilizokuwepo walihifadhiwa katika kanzidata (Database) ambayo hudumu kwa  muda cha miezi sita (6) baada ya matokeo ya usaili husika kutolewa.
Baada ya ufafanuzi huo hususani aya ya tatu Sekretarieti ya Ajira ingependa kufafanua zaidi namna kanzidata ya waliofaulu usaili inavyotumika ili kuweza kuwa na uelewa wa pamoja kwa wadau na jamii kwa ujumla ili kuepusha kupokea ama kusikia taarifa  zisizo rasmi zenye nia ya kupotosha Umma zinazojitokeza mara kwa mara hususani katika baadhi ya mitandao ya kijamii.
Kanzidata ya waliofaulu  usaili:
Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa shughuli za Sekretarieti ya Ajira za mwaka 2016, Kanuni ya 21. (1) - (5) imefafanua juu ya kanzidata kama ifuatavyo;-
(1) Baada ya waombaji waliofaulu usaili kuwapangia vituo vya kazi, orodha itakayobaki itatunzwa na Katibu katika kanzidata ili pale itakapotokea fursa ya ajira orodha hiyo iweze kutumika.
(2) Orodha ya waombaji walioko kwenye kanzidata itatumika kujaza nafasi wazi kulingana na mahitaji ya Waajiri. Hata hivyo, wakati wa upangaji, Katibu atazingatia mpangilio wa matokeo ya alama za ufaulu wa mwombaji kwa aliyepata alama za juu zaidi ya wengine kufikiriwa kwanza.
(3) Sekretarieti itatangaza nafasi wazi za ajira na kufanya usaili endapo orodha iliyotunzwa katika kanzidata itakuwa imekwisha au haina mtumishi mwenye utaalam au sifa zinazohitajika na Mwajiri.
(4) Endapo katika orodha iliyotajwa kwenye Ibara ya 21(2) kutakuwa na waombaji waliopata alama zinazolingana, utaratibu ulioainishwa katika Ibara ya 14(1) utazingatiwa.
(5) Orodha ya kanzidata itadumu kwa kipindi cha miezi sita (6) tangu kuidhinishwa kwa matokeo na Wajumbe wa Sekretarieti.
2.       Sekretarieti ya Ajira pia inapenda kutoa ufafanuzi kwa taarifa nyingine iliyoandikwa katika mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari kinachosema “Mhe Rais Magufuli nakuomba Sekretarieti ya Ajira uifute maana haina majukumu sasa hivi lengo la Sekretarieti ya Ajira ni kutangaza kazi na ........”. kama ifuatavyo;-
Ni vyema wadau wa Sekretarieti ya Ajira na Jamii kwa ujumla ikafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ilianzishwa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (1). Kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu cha 29 (6) (a-f) na Sera ya Menejimenti ya Ajira toleo Na. 2 la mwaka 2008 Sekretarieti ya Ajira ina majukumu yafuatayo;-
i.        Kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa (kanzidata) za wataalam hao ili kurahisisha utaratibu wa kuwaajiri pindi wanapohitajika,
ii.       Kuandaa orodha ya wahitimu wa Vyuo Vikuu na Wataalam Weledi (Professionals) kwa madhumuni ya kurahisisha rejea na ujazaji wa nafasi wazi za ajira katika Utumishi wa Umma,
iii.      Kutangaza nafasi wazi za kazi zinazotokea katika Utumishi wa Umma.
iv.      Kuhusisha wataalam maalum (Appropriate experts) kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji,
v.       Kutoa ushauri kwa Waajiri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na ajira,
vi.      Kufanya kazi nyingine yoyote inayoendana na majukumu yake kadri itakavyoelekezwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma.
Kutokana na ufafanuzi huo Sekretarieti ya Ajira ingependa jamii ifahamu mbali na jukumu la kuendesha mchakato wa Ajira ina majukumu mengine inayoyatekeza kama yalivyoainishwa hapo juu kwa mujibu wa Sheria.

Riziki V. Abraham
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Sekretarieti ya Ajira.
27 Desemba, 2016.
Share:

MWALIMU ASHUSHIWA KIPIGO KWA KUMCHARANGA MAPANGA MWANAFUNZI WAKE SIKU YA KRISMASI



Kijana Limbe akipata matibabu
Mwalimu Pendo akipata matibabu
*****

MWANAFUNZI Marco Limbe(14) aliyemaliza darasa la saba mwaka huu katika shule ya msingi Yitwimila iliyoko kata ya Kiloleli wilaya ya Busega mkoani Simiyu amelazwa katika kituo cha afya Busega mara baada ya kuchalangwa mapanga kichwani na mdomoni na mwalimu wake.



Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 11.30 jioni wakati mwanafunzi huyo alipokuwa akirejea nyumbani kwao akitokea katika malisho ya mifugo,alipokaribia katika shamba la mwalimu Pendo Gabriel ndipo mwalimu huyo alimkamata kijana huyo na kuanza kumcharanga kwa panga na kusababisha kijana Limbe kupoteza fahamu kwa muda wa masaa 6.

“Shuhuda wa tulio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Manoga anasema ilikuwa kama mchezo lakini kumbe ni kweli kwani niliona mifugo ya Limbe iliyokuwa ikielekea nyumbani na huku Limbe akiwa nyuma ya mifugo hiyo katika barabara ambayo iko karibu na maeneo ya shule, ghafla nilimuona mwalimu Pendo wakishikana na kijana huyo na ndipo nikamuona akiwa na panga na kuanza kumcharanga”,alieleza.
"Nilikimbia katika tukio na kutoa msaada kwa wote lakini, watu walijaa na kuanza kumshambulia mwalimu Pendo kwa kumpiga ingawa jaribio hilo lilikwama baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho Mshemas Bahai.
Mwandishi wa habari hizi alikwenda katika kituo cha afya cha Nyashimo na kujionea hali mbaya kwa kijana Limbe ambaye alikuwa amepoteza fahamu kwa muda wa masaa 6 bila kujitambua na huku akiwa anaongezewa drip na kwa pembeni mwalimu Pendo Gabriel naye akipata matibabu ya jeraha lake kichwani ambAlo alishambuliwa na wananchi na huku akiwa chini ya ulinzi wa jeshi la polisi.
Mwenyekiti wa Sogesca Bahai Mshemas alisema sikukuu Krismasi imekuwa ni mbaya katika kijiji chake baada ya wananchi wenye hasira kali kufanya shambulio la kumshambulia mwalimu Pendo kwa kosa la kumcharanga na panga mwanafunzi wake aliyekuwa akitokea kwenye malisho na kupita karibu na shamba lake la mahindi akitokea katika malisho.
Hata hivyo alisema alifanikiwa kuwatuliza wananchi wa kijiji chake na kuanza kufanya mikakati ya kuwapeleka kituo cha afya ili wapate huduma za matibabu.
Aliongeza kuwa walifika polisi na kuandikiwa barua ya kwenda kutibiwa wote wawili mwalimu pamoja na mwanafunzi.
Kwa upande wake kaimu mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya Dk. Ayubu Ismail alithibitisha kuwapokea kwa majeruhi hao na kudai kuwa kijana Limbe ndiye aliyekuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwalimu Pendo.
Aliongeza kuwa kijana ameshonwa nyuzi 9 katika sehemu zake zote alizopatwa na majeraha na huku mwalimu  akishonwa nyuzi 6.
“Ni kweli Limbe alikuwa ametokwa na damu nyingi sana na hivyo kumpelekea kupoteza fahamu kwa muda wa masaa 6 lakini hali yake inaendelea vizuri alisema Dk. Ismail”.
Na Shushu Joel- Busega
Share:

NYOKA WA MAAJABU AFA NA MTU WAKE,ALIKUWA AMEMBEBA KWENYE NGUO YAKE



DUNIANI kuna mambo, ndivyo unaweza kusema kutokana na mkazi wa Mtaa wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) kufa baada ya nyoka wake aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma (Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa. Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile majeraha au vifo.
Aidha katika tukio lingine, mkazi wa kijiji cha Mdunduwalo Joseph Charles (27) amefariki dunia kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali tumboni na Oddo Komba (34) mkazi wa Mhepai Peramiho baada ya kuhitilafiana wakati wakitoka kunywa pombe.
Kamanda huyo wa polisi alisema, tukio hilo limetokea tarehe 26 mwezi huu saa 1 usiku katika kijiji cha Mtyangimbole kata ya Gumbiro katika halmashauri ya wilaya ya Madaba wilayani Songea ambapo chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliotokea njiani kati yao wakati wakirudi nyumbani kutoka kwenye klabu za pombe ya kienyeji.
IMEANDIKWA NA MUHIDIN AMRI- habarileo SONGEA
Share:

MWANAFUNZI APIGWA RISASI KWENYE MGOGORO WA NYUMBA


Mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya sekondari Mringa, Vanessa Josephat [16] mkazi wa Sakina jijini Arusha amejeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi kichwani na walinzi wa kampuni ya ulinzi ya kifaru waliokuwa wakiwatoa kwa nguvu kwenye nyumba yao yenye mgogoro .
Tukio hilo limethibitishwa na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha Charles Mkumbo ambaye alisema kuwa polisi inamshikilia Fabian Charles mlinzi wa kampuni ya kifaru pamoja na silaha aina ya shoot gun iliyo tumika katika tukio hilo huku majeruhi amelazwa katika hospitali ya KCMC kutokana na hali yake kuwa mbaya .
Kamanda mkumbo alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa tatu asubuhi katika eneo la sakina jijini hapa, ambapo alisema walinzi watatu wa kampuni hiyo waliokuwa wakilinda nyumba hiyo inayomilikiwa na Josephat Nehemia walitumia silaha hiyo kuwafyatulia familia inayoishi hapo ili waondoke na ndipo silaha hiyo ilipomjeruhi mwanafunzi huyo .
Taarifa zinaeleza kuwa December 21 mwaka huu kampuni ya udalali ya Marc Recorders Limited wakiwa na mabaunsa na watu wengine walivamia nyumba hiyo na kuwatoa nje wamiliki wa nyumba hiyo na kuondoka na vyombo vyao vya ndani wakidai nyumba hiyo imeshauzwa kwa , Thobias Ludovick Senya baada ya mmiliki kushindwa kulipa deni la shilingi million 3.7 alilokuwa akidaiwa na taasiai ya fedha Heritage.
Baada ya tukio hilo familia hiyo yenye watu wapatao kumi wakiwemo watoto na kichanga walianza kulala nje kando ya geti la nyumba hiyo wakipigwa na baridi kali pasipo kuwa na msaada wowote
Mmiliki wa nyumba hiyo Josephat Nehemia Ogaga alisema baada ya familia yake kutolewa nje wakati yeye akiwa safarini walikuja walinzi hao wa kampuni ya kifaru na kuanza kulinda na baada ya yeye kurejea alifanikiwa kuwaondoa walinzi hao na kuirejesha ndani familia yake akidai taratibu za kuuza nyumba yake hazikufuatwa ila kilichofanyika ni uhuni .
“Nikweli nilikuwa nadaiwa na Heritage financial shilingi milioni 3 .7 na nililipa deni na kubaki shilingi million 1.8 hivyo hatua ya kuja kuuza nyumba yangu yenye thamani shilingi million 200 kwa deni hilo ni uhuni mtupu umefanyika” alisema Nehemia
Hata hivyo siku moja baadae walinzi hao walirejea tena wakiwa na silaha za moto na kuanza kufyatua risasi ovyo ndani ya nyumba hiyo kwa lengo la kuwatisha familia hiyo ili waondoke ndani ya nyumba hiyo ambapo moja ya risasi ilimjeruhi mwanafunzi huyo kichwani ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu
Kamanda Mkumbo amezitaka kampuni za ulinzi kutoingilia migogoro bila kufuata utaratibu kwani vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia migogoro kama hiyo vipo na hivyo amezitaka kampuni za ulinzi kufuata taratibu zao za utendaji wa kazi na kuacha kukimbilia maslahi yao ya kupata fedha haraka,
Mkumbo alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Share:

Waziri Mkuu: Waliofaulu Ni Lazima Waende Sekondari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitavumilia kuona mamia ya vijana waliofaulu mitihani ya darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanabaki nyumbani eti kwa kuwa hakuna madarasa ya kutosha.

“Serikali haitaridhika kuona vijana waliofaulu vizuri wanashindwa kwenda kidato cha kwanza. Halmashauri zilijua tangu mapema ni wanafunzi wanaenda shule za msingi kwa hiyo inataka kuona wote waliofaulu wanakwenda sekondari kwa asilimia 100,” amesema.

Ametoa kauli hiyo jana  mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea. Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapunziko ya mwisho wa mwaka.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutoa elimu ya bure kwa kila mtoto sasa iweje watoto wengine wanafaulu na wanashindwa kujiunga na elimu ya sekondari. 
“Tumesema elimu ni bure hakuna sababu ya kufanya wengine wasiende shule wakati azma ya Serikali ni kutoa elimu ya bure. Hakikisheni wote wanaingia katika chaguo la kwanza,” alisema.

Aliwataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimefaulisha wanafunzi lakini hazina madarasa na madawati ya kutosha warudi mezani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanapangwa na kuanza na wenzao katika chaguo la kwanza kwani wakisubiri chaguo la pili wanakuwa wamechelewa.

“Kama tumepokea vijana wengi kwenye udahili wa kidato cha kwanza, ni dhahiri kuwa ,tutapata Vijana wengi watakaomaliza kidato cha nne. Sote tunajua kuna agizo la kila tarafa kuwa na sekondari moja ya kidato cha tano na sita, nataka utekelezaji wa agizo hili usimamiwe kuanzia sasa.”

“Tafuteni moja kati ya shule kwenye tarafa zenu na ipandishwe hadhi kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa ya bwalo, jiko, mabweni, mifumo ya maji, madarasa na vyoo vya kutosha,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema atafuatilia ili abaini ni kwa nini taasisi ya maghala ya Serikali inadai tozo kwa wakulima wanaohifadhi mazao kwenye maghala hayo.

Waziri Mkuu alisema atapitia sheria ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ili kuona kama inaruhusu tozo hizo na kuangalia sheria gani inawaruhusu kutoza kodi. Alihoji inakuwaje taasisi ya Serikali inatoza tozo kwenye maghala ambayo yamejengwa na wananchi.

Akitoa mfano kuhusu ghala la Liwale, Waziri Mkuu alisema: “Kuna viagency vimeanzishwa kazi yao ni kutoza mapato tu. Inakuwaje kunakuwa na taasisi imekaa tu na kuanza kutoza tozo kwa wananchi wanaotumia facility za Serikali. Sheria ya kutoza tozo imetokana na nini na hizo zinakwenda kwa nani, je srikali imeanza kufanya biashara?,” alihoji.

“Nimepata taarifa kuwa walikuja kuzuia mazao yasitoke hadi wao walipwe, hapana huu siyo utaratibu. Ni kwa nini tuwanyang’anye fedha wale waliojenga ghala? Wao walijenga ghala kutokana na ubunifu halafu unasema unawapa sh. 7/- kwa kilo wakati wewe umetoza sh.25/- kwa kilo moja. Hapana hilo halikubaliki,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema kama Serikali inaruhusu kuwepo kwa tozo hizo kwa jambo ambalo wananchi wamelibuni wenyewe, basi ilipaswa kudai kodi na hiyo kodi ilitakiwa kukusanywa na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na siyo vinginevyo.

Waziri Mkuu alisema atafuatilia wakala mbalimbali walioanzishwa kwenye wizara kwani kuna nyingine zinafanya kazi ambazo zilistathili kufanywa na idara kwenye wizara mama.
    
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger