Friday 22 January 2021

HAYA NDIYO MATAIFA 10 BARANI AFRIKA YENYE PASIPOTI ZENYE UWEZO MKUBWA

...

Mwaka 2021 unapojiandaa kusafiri kwa kutumia pasi yako ya kusafiria ni vyema kujua ni wapi pasi ya nchi yako inaweza kukupeleka.

Jinsi pasi ya kusafiria ya taifa lako inavyoweza kukuingiza katika mataifa mengi bila kutumia visa ndivyo jinsi kibali hicho kilivyo na uwezo.

Kila miezi mitatu kulingana na mtandao wa BBC Pidgin, Shirika la Henley Passport Index linashirikiana na shirika la usafiri wa kimataifa IATA ili kuripoti kuhusu uwezo wa pasipoti ya kila taifa wakati wa usafiri bila kutumia visa.

Katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 shirika hilo limetoa idadi ya mataifa 10 yalio na pasipoti zenye uwezo mkubwa barani Afrika.

Pasipoti zenye uwezo mkubwa barani Afrika
Katika orodha hiyo taifa la Sycheles ndilo lenye pasipoti yenye uwezo mkubwa barani Afrika ikiwa na uwezo wa kukuingiza katika mataifa 151 bila kutumia Visa.

Katika nafasi ya pili, ni nchi ya Mauritius ambayo kibali chake cha usafiri kinaweza kukusaidia kuingia katika mataifa 142 bila kutumia Visa.

Taifa la tatu ni lile la Afrika Kusini ambalo unapoitumia pasipoti yake inaweza kukupeleka katika mataifa 101 bila kutumia visa.

Nafasi ya nne katika orodha hiyo ni taifa la Botswana ambalo pasipoti yake inaweza kukuingiza mataifa 85 bila kutumia visa.

Mataifa mengine yenye pasipoti zinazokaribiana kwa uwezo ni pamoja na Namibia, Lesotho, Eswatini na Malawi.

Pasi ya taifa la Nigeria inaweza kukuingiza katika mataifa 46 bila kutumia visa duniani, huku ile ya Ghana ikiwa na uwezo wa kukupeleka katika mataifa 65 nayo ya Cameroon ikikusafirisha na kukuingiza katika mataifa 49 bila ya kutumia visa.

Habari za hivi karibuni kuhusu pasi kumi zenye uwezo mkubwa Afrika zinaonesha kwamba Kenya ilishuka katika orodha hiyo na kuwa nambari 11.

Afrika mashariki

Kenya
Kulingana na mtandao huo wa Henley Index ,uwezo wa pasi ya Kenya umepungua katika miaka ya hivi karibuni kutoka nafasi ya 52 mwaka 2006.Taifa hilo la Afrika mashariki kwa sasa lipo katika nafasi ya 73 duniani huku wale wanaotumia pasi yake wakiwa na uwezo wa kuingia mataifa 72 pekee duniani.


Tanzania
Tanzania ni taifa la Afrika mashariki lenye sifa ya vivutio vya kitalii kama vile mbuga ya Serengeti na mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu barani Afrika. limeorodheshwa kuwa taifa la 74 katika mtandao huo wa Henley index huku wanaomiliki pasi yake wakiwa na uwezo wa kuzuru mataifa 71 duniani bila kutumia visa.

Pasipoti zenye uwezo mkubwa duniani
Katika miaka mitatu mfululizo pasipoti ya Japan inasalia nambari moja kama pasi yenye uwezo mkubwa dunia ikiwa na uwezo wa kukuingiza katika mataifa 191 kote duniani bila kutumia visa.

Miaka michache iliopita walikuwa wakishikilia uwezo huo sawa na Singapore.

Hata hivyo Singapore imeshuka nafasi moja chini na kuwa nambari mbili huku pasi yake ikiwa na uwezo wa kukuingiza katika mataifa 190 duniani bila kutumia visa.

Korea Kusini na Ujerumani zinashikilia nafasi ya tatu kwa pamoja.

Mataifa matatu ambayo pasipoti zao zina uwezo wa chini duniani ni Syria, Iraq na Aghanistan.

CHANZO - BBC SWAHILI

Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger