Friday 23 October 2020

Majanga ya moto yasiwe sababu za kuirudisha kada ya elimu.

...


Samirah Yusuph,

Simiyu. Kufuatia uwepo wa tetesi za kuzuiliwa kwa makambi ya elimu mashuleni kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi na wenye madarasa ya mtihani, Mkuu wa mkoa wa simiyu Anthony Mtaka ametoa tamko la kuendelea na makambi kama ilivyokuwa hapo awali.

Ambapo aliwataka walimu kuendelea na maandalizi ya makambi hayo ambayo yatafunguliwa rasmi tarehe 30 mwezi huu huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika makambi ili kuhakikisha usalama wakati wote.

Mtaka alielekeza walimu kuendelea na mikakati ambayo walijiwekea awali ili kuhakikisha wanafunzi wanapata muda zaidi wa kufanya mitihani ya majaribio, ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuinua hali ya ufauru mkoani hapo.

"Tupo pale pale hakuna kurudi nyuma ili kuhakikisha tunaendelea kuinua kiwango cha ufauru kwa watoto wetu, na jamii inatakiwa kuwekeza zaidi katika elimu, hivyo ninaruhusu makambi yaendelee kwa manufaa ya hawa wanafunzi,"  alisema Mtaka na kuongeza kuwa:

"Wanafunzi wa kike watakao kuwa katika makambi hayo watapatiwa tauro za kike bure ili kuwaongezea ufanisi zaidi wa kuzingatia masomo yao, na zawadi zipo zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa walimu na wanafunzi watakao fanya vizuri kwenye masomo yao,".

Makambi hayo yametajwa na baadhi ya wanafunzi kuwa yamekuwa ni msaada kwa wanafunzi waishio katika mazingira magumu pamoja na wale wa maeneo ya vijijini kwani wanapokuwa katika makambi inakuwa ni rahisi kwao kuwa na muda mwingi wa kusoma.

Hali ambayo imefafanuliwa na Nicholaus John mwanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi kuwa kurudishwa kwa makambi ni furaha kwao kwani ingewapoteza katika umoja wa kujisomea.

"Tunapokuwa katika makambi tunapata muda wa kujisomea na kukadili kwa pamoja kuhusu masomo hivyo inakuwa ni rahisi sana kwetu kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea," alisema.

"Kwa watoto wa kike ni msaada zaidi kwani kunawengine huwa hawaonekani kwenye vyumba vya mtihani kwa sababu ya changamoto za nyumbani lakini tunapokuwa kwenye makambi inatupa uhakika wa wote kufanya mtihani na kuongeza bidii za kusoma," aliongeza Nshoma Joseph.

Huku mwenyekiti wa kamati ya taaluma iliyoundwa kwa dhumuni la kuwainua wanafunzi kitaaluma mkoani hapo Khamis Lubugwa alisema kuwa lengo ni kuongeza ufauru kwa kuwapatia muda zaidi wa kujisomea na kujiandaa wanafunzi wanaokuwa katika madarasa ya mitihani.

"Hii inaweka usawa wa watoto kupata elimu kwani kuna baadhi wanatoka katkka mazingira magumu na inakuwa ni ngimu kwao kupata nafasi na muda wa kutosha kwa ajili ya kujisomea," alitanabahisha.

Aidha afisa elimu mkoa wa Simiyu  Erenest Hinju alifafanua kuwa maandalizi ya makambi kwa wanafunzi wa kidato cha nne, tayari yameanza kufanyika na yapo katika hatua za mwisho kuweza kakamilika na wanafunzi watakuwa makambini kuanzia tarehe 30 mwezi huu hadi novemba 27.

Mwisho.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger