Friday 18 September 2020

Majaliwa: Tumchague Dkt. Magufuli, Tusijali Itikadi Za Vyama Vyetu

...


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waweke kando itikadi zao za vyama na wamchague mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu maendeleo hayachagui chama.

Ametoa wito huo jana (Alhamisi, Septemba 17, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Lagangabilili, wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Lagangabilili.

Amesema Dkt. John Pombe Magufuli, anastahili kupewa kura zote kwa sababu amefanya makubwa na anastahili apewe miaka mitano mingine akamilishe kazi nzuri aliyoianzisha.

Akielezea yaliyofanyika chini ya Ilani ya CCM kwenye sekta ya miundombinu, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 3.2 zimetolewa kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwemo barabara za kutoka Chinamili-Nanga; Budalabujiga-Mitobo-Nguno; Lagangabilili-Migato-Ndoleleji na Inalo-Mahembe-Sawida.

Barabara nyingine zilizofanyiwa matengenezo ni Bulolambeshi – Bumera - Ndoleleji; Itilima Oil-Chinamili – Ikindilo; Gambasingu – Nkoma - Mwamapalala; Mwamapalala -Bukingwaminzi – Kinang’weli na Mwaswale – Laini – Nanga yakiwemo makalvati na madaraja 171.

Kwa upande wa elimu, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.87 zilitolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya nyumba za walimu, vyoo na madarasa kwa shule za msingi ikiwemo shule za Ngeme, Mahembe, Sawida A, Gambasingu 'A', Kidula, Mlimani, na Ikindilo.

“Kwenye shule za sekondari, zilitolewa shilingi bilioni 1.87 nyingine kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mabwalo, maabara, mabweni, matundu ya vyoo na madarasa kwa sekondari za Itilima, Kanadi, Lagangabilili na Bunamhala Mbugani.”

Alisema ili kuwawezesha wananchi wafanye shughuli za kilimo na ufugaji bila bugudha, Rais Magufuli aliagiza vijiji 920 kati ya 975 ambavyo vilikuwa vina migogoro ya matumizi ya ardhi na Hifadhi za Taifa, mashamba, ranchi, mapori ya akiba au vyanzo vya maji visiondolewe katika maeneo vilipo na taratibu za kuvirasimisha ziendelee.

Aidha, aliruhusu maeneo ya hifadhi ya misitu na mapori ya akiba yasiwe na eneo la kinga la mita 500 (Buffer Zone) na kusisitiza kwamba ni hifadhi za taifa tu ndizo zitakazokuwa na maeneo ya kinga ya mita 500 (Buffer Zone).

Kufuatia uamuzi huo, maeneo ya kinga ya Hifadhi za Taifa ambayo yalivamiwa iliamriwa kuwa yataachwa kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Alisema vijiji vya Wilaya ya Itilima ambavyo vinabaki katika eneo kinga la mita 500 kutoka mpaka wa hifadhi ya Serengeti ni pamoja na; Mbogo, Pijulu, Mwamakili, Ng’walali, Nyantugutu, Shishani, Ndingh’o na Longalambogo.

Alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Itilima, Bw. Njalu Silanga, mgombea udiwani wa kata ya Ligangabilili, Bw. Doto Nyasama na wagombea udiwani wa kata zote za wilaya ya Itilima waliokuwepo kwenye mkutano huo.


Share:

0 comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger